Katika juhudi za kuwaenzi wanamichezo walioliletea
sifa kubwa taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kamisheni ya Ngumi za
Kulipwa Nchini (TPBC) iko kwenye mchakato wa kuanzisha Taasisi ya Michezo ya
Rashid Matumla (Rashid Matumla Sports Academy) ya kuibua vipaji vya vijana
wanaochipukia katika michezo hususan ngumi.
Huu ni mkakati wa kumwandaa bingwa wa zamani wa dunia
aliyetambuliwa na Umoja wa Ngumi wa Dunia (Rashid Matumla) kustaafu ngumi ili
aweze kutumia kipaji chake cha ngumi kuendeleza vijana.
TPBC inajivunia historia nzuri ya Rashid Matumla kwa
kuwa bondia wa kwanza Tanzania kuwa bingwa wa dunia aliyetambuliwa na Umoja wa
Ngumi wa Dunia (WBU) pamoja na sifa kemkem alizoliletea taifa hili kipindi hiki
chote anachopigana ngumi. Tunapenda kuutangazia umma kuwa tunamwandalia Rashid
Matumla mazingira mazuri ya kustaafu ngumi.
Katika taasisi hiyo ya Rashid Matumla Sports Academy,
Rashid atakuwa ndiye Rais na atakuwa analipwa mshahara kama mwajiriwa kwa
kipindi chote cha uhai wa taasisi hiyo na kumfanya aweze kujipatia ajira ya
kudumu wakati hachezi tena ngumi. Huu ni moja ya mikakati ya TPBC kuhakikisha
kuwa mabondia wake walioiletea nchi hii heshima kubwa wanaenziwa kwa kuandaliwa
maisha mazuri wanapostaafu ngumi!
Ni lazima kama taifa tuwajali wale wote wanaolipigania
taifa hili na tutaendelea pia kuandaa mazingira mengine ya kuwawezesha waishi
vizuri na kuheshimiwa daina ili kuleta changamoto kwa wengine ili nao wapigane
kufa na kupona kuliletea sifa taifa letu katika michezo.
Taasisi hii itazinduliwa rasmi wakati wa mpambano wa
Rashid Matumla na Vitaly Shemetov bondia anayetoka Urusi litakalofanyika mjini
Moshi tarehe 22nd Juni na kuhudhuriwa na Mcheza sinema maarufu wa Marekani,
Deidre Lorenz wa sinema maarufu ya Santorini Blue. Mcheza sinema huyo atakuwepo
nchini kwa ajili ya kukimbia mbio za Marie Frances Mt. Kilimanjaro Marathon
kusheherekea miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika zikazofanyika tarehe 24 Juni mwaka
huu kuanzia Moshi Club.
Taasisi ya Rashid Matumla Sports Academy ambayo
itakuwa inafanya kazi nchi nzima itajumuisha pia bingwa mwingine wa zamani wa
dunia aliyetambuliwa na Umoja wa Ngumi wa Dunia (WBU) Magoma Shaban. Hawa wote
watakuwa waajiriwa wa taasisi ya Rashid Matumla Sports Academy wakifanya kazi
za kuibua vipaji kwa vijana Tanzania nzima!