Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
linaendelea na mpango wake wa kuwaendeleza waamuzi watoto wa Kituo cha Kambi ya
Twalipo kilichoko Mgulani jijini Dar es Salaam kwa kuwapa mafunzo zaidi na
kuwatumia katika mashindano mbalimbali.
Lengo ni kuboresha uwezo wao
katika kuchezesha mchezo wa mpira wa miguu na kutoa changamoto kwa vijana wadogo
wengine, hasa wa shule za msingi, sekondari na wanafunzi wa vyuo vya elimu ya
juu kuingia katika uamuzi ili kujenga kizazi kipya katika fani
hiyo.
Wazo la kuwa na waamuzi
watoto lilianzia kwa Meja Bakari wa kituo hicho, juhudi ambazo TFF inazipongeza
na kuziunga mkono kwa kutoa mafunzo zaidi kwa wahusika. Wiki mbili zilizopita
tuliwaandalia mafunzo zaidi ya kuwanoa ambayo yaliendeshwa na Mkufunzi wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Leslie Liunda.
TFF imeshawatumia waamuzi hao
watoto katika mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Kombe la Uhai),
michuano ya vijana ya Rollingstone iliyofanyika jijini Arusha na fainali za Copa
Coca-Cola. Mashindano yote hayo yalifanyika mwaka jana na kiwango walichoonesha
waamuzi hao kilikuwa kizuri.
Hivyo tutaendelea kuwapa
mafunzo zaidi na mashindano mengine kadri tutakavyoona inafaa kwa lengo la
kuwajenga na kuwaongezea ujuzi.