KOCHA mkuu wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu soka Tanzania Bara, Yanga Kostadin Papic anadaiwa kuchangia timu hiyo kupoteza mchezo baina ya timu hiyo na Toto African ya Mwanza iliyopigwa jumapili kwenye dimba la CCM Kirumba ambapo Yanga ilipokea kichapo cha mabao 3-2.
Taarifa ambazo mamapipiro blog imezipata zinaeleza kwamba kocha huyo mwenye vituko aliushangaza uma pindi alipoibuka siku ambayo timu inashuka dimbani na kuamua kubadili kikosi kilichopangwa na kocha msaidizi,Fred Felix Minziro.
"Huyu kocha anashangaza yeye alijifanya anaumwa na kubaki Dar es Salaam kwa zaidi ya siku tatu, lakini aliibuka siku ya mchezo na kwenda kupangua kikosi kilichopangwa na mwenzake sasa kwa hali hii nani wa kulaumiwa,"Alisema mtoa habari huyo.
Imeelezwa kuwa Papic alitumia mamlaka yake kumuondoa katika kikosi kipa namba moja Yaw Berko na kumuweka Shaban Kado kitu ambacho hakikuwa sahihi kwani Minziro alikaa na wachezaji na hivyo kuona ni nani anastahili kuanza na nani anastahili kukaa benchi.
Kufuatia kipigo hicho Yanga imejiweka katika mazingira magumu ya kutetea ubingwa kwani imeendelea kubaki na pointi 43 nyuma ya Azam yenye pointi 50 na vinara wa ligi hiyo Simba wenye pointi 53.
Yanga inatarajiwa kushuka dimbani kesho kukwaana na Kagera Sugar ya Kagera katika mchezo utakaopigwa kwenye dimba la Kaitaba mjini Bukoba, ambapo baada ya mchezo huo iytakuwa imebakiza michezo miwili kabla ya ligi kumalizika.