Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za
Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ilikutana Mei 26 mwaka
huu ili kutoa mwongozo wa nini kifanyike ndani ya Yanga baada ya wajumbe wake
kudhaa kujiuzulu.
Kamati ya Uchaguzi ya Yanga ilikuwa imeomba mwongozo huo
TFF.
Baada ya kupata taarifa rasmi
kutoka Yanga, Kamati imebaini kuwa Kamati ya Utendaji ya Yanga imekosa akidi
baada ya wajumbe wake wengi kujiuzulu hivyo kutokuwa na uwezo wa kufanya uamuzi
kwa mujibu wa Ibara ya 32(1) ya Katiba ya klabu hiyo.
Hivyo, Kamati imetoa mwongozo
kwa Kamati ya Uchaguzi ya TFF ambayo ndiyo msimamizi wa Kamati ya Uchaguzi ya
Yanga kuwa ili Kamati ya Utendaji ya Yanga iwe na nguvu za kikatiba kufanya
shughuli zake ikiwemo uamuzi wa masuala mbalimbali ndani ya klabu hiyo ni lazima
iwe na akidi.
Kwa mujibu wa Ibara ya 29(3)
ya Katiba ya Yanga nafasi zilizo wazi katika Kamati ya Utendaji zinatakiwa
kujazwa katika Mkutano Mkuu wa Kawaida ujao.
Pia Kamati imebaini uteuzi wa
kujaza nafasi zilizo wazi za wajumbe uliofanywa na Kamati ya Utendaji ya Yanga,
Mei 21 mwaka huu ni batili kwa vile Kamati ya Utendaji iliyofanya uteuzi huo
haikuwa na akidi.
Ili kupata akidi na kufanya uamuzi Kamati
ya Utendaji ya Yanga yenye wajumbe 13 inatakiwa kuwa na asilimia 50 ya wajumbe
wote, hivyo ili wafanye uamuzi halali hawatakiwi kupungua saba.
Kwa wajumbe ambao
hawajajiuzulu; Sarah Ramadhan, Mohamed Bhinda, Tito Osoro na Salim Rupia kwa
sasa hawawezi kufanya shughuli zozote za Yanga hadi nafasi zilizo wazi katika
Kamati ya Utendaji zitakapojazwa.
Kama inavyoelekeza Katiba ya
Yanga, shughuli za kila siku za klabu hiyo zitaendelea kufanywa na Sekretarieti
ya Yanga ambayo kiongozi wake ni Katibu Mkuu.
Alex
Mgongolwa
Mwenyekiti
Kamati ya
Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji