Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea Hati
ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ya mchezaji George Odhiambo 'Blackberry' , raia wa Kenya
aliyejiunga na klabu ya Azam.
Hati hiyo imetolewa na Chama cha Mpira wa Miguu cha Denmark
(DBU) ambapo Odhiambo alikuwa akicheza nchini humo kabla ya kutua Azam kwa
ajili ya msimu wa 2012/2013.
Klabu nyingine zinazosajili wachezaji kutoka nje ya Tanzania
zinatakiwa kuhakikisha zinakamilisha uhamisho wao (transfer) kabla ya Julai 30
mwaka huu ambayo ndiyo siku ya mwisho kufanya hivyo.
Kanuni ya 41 ya Ligi Kuu kuhusu ITC inasema: “(1) Maombi ya
ITC kwa wachezaji wa kigeni wa kulipwa yatawasilishwa kupitia mtandao wa
kompyuta kwa kutumia program ya ‘Transfer Matching System-TMS’ baada ya klabu
zinazohusika na mchezaji huyo au wachezaji hao kukubaliana nje ya mtandao.
(2) Maombi ya ITC kwa wachezaji wa kigeni wasio wa kulipwa
yatawasilishwa kwa barua TFF baada ya klabu zinazohusika na mchezaji huyo au
wachezaji hao kukubaliana. Chama cha Soka kinachotoa ITC kwa njia hii
kitapeleka nakala FIFA. (3) ITC haihitajiki kwa mchezaji mwenye umri chini ya
miaka kumi na mbili (12).”
Tunapenda kuzikumbusha klabu kuwa kwa mujibu wa Kanuni ya 53
ya Ligi Kuu, wachezaji wa kigeni ni lazima wawe wanachezea timu ya Taifa au
klabu za Ligi Kuu huko wanakotoka.
Kanuni hiyo inasema: “Klabu inaruhusiwa kusajili wachezaji
wa kigeni wa ngazi ya kimataifa ambao ni wa timu za Taifa na Ligi Kuu kutoka
nje ya nchi wasiozidi watano (5). Wachezaji kutoka Ulaya na Marekani ya Kusini
wanweza kuwa wa daraja la pili na kuendelea, na klabu inaruhusiwa kuchezesha
wachezaji walioorodheshwa wasiozidi watano (5) wa kigeni katika mchezo mmoja.
Wachezaji hao watasajiliwa baada ya TFF kuhakikisha usahihi wa taarifa zao na
kukamilika kwa taratibu za uhamisho wa kimataifa.”