Kamati ya Uchaguzi ya TFF, kwa kuzingatia majukumu yake ya
kusimamia chaguzi za wanachama wa TFF kama
ilivyoanishwa kwenye Katiba ya TFF, Ibara ya 49 (1), na Kanuni za Uchaguzi za
wanachama wa TFF Ibara ya 26(2) inatoa ufafanuzi ufuatao kuhusu uchaguzi wa kuziba
nafasi za uongozi kwenye Klabu ya Yanga:
1. Wanachama
wote wa TFF, ikiwa ni pamoja na Klabu ya Yanga, wanatakiwa kuzingatia
kikamilifu Kanuni za Uchaguzi za
Wanachama wa TFF katika kuendesha shughuli zote za uchaguzi.
2. Wagombea
uongozi wote wa wanachama wa TFF wanapaswa kutimiza masharti ya uongozi
yaliyoanishwa katika Katiba za vyama vyao na Kanuni za Uchaguzi.
3. Kamati za
Uchaguzi za Wanachama wa TFF zinapaswa kutimiza kikamilifu majukumu yao ya kulinda Katiba za
wanachama wa TFF na kuzingatia Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF katika
michakato ya uchaguzi. Kamati ya Uchaguzi ya Yanga ilishaelekezwa kufanya hivyo
na inakumbushwa kuendelea kuzingatia wajibu huo.
4. Wagombea
uongozi wa wanachama wa TFF wanao wajibu wa kuzifahamu Katiba zao na Kanuni za
Uchaguzi za Wanachama wa TFF na kuomba uongozi kwa kutimiza matakwa ya Katiba
na Kanuni za Uchaguzi.
5. Kamati ya
Uchaguzi ya TFF imepokea maombi ya marejeo (review) dhidi ya uamuzi wake wa
kuwaondoa waombaji uongozi wanne (4) wa Klabu ya Yanga. Kamati ya Uchaguzi ya
TFF inatoa uamuzi ufuatao:
i) Marejeo
yaliyoombwa na Kamati ya Uchaguzi ya Yanga yanakiuka Kanuni za Uchaguzi za
Wanachama wa TFF, hivyo Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeyakataa. Kamati inafafanua
kuwa hata kama Kanuni zingekuwa zinaruhusu
kufanya marejeo, bado maombi hayo yasingepaswa kuwasilishwa na Kamati ya
Uchaguzi ya Yanga, bali waombaji uongozi wenyewe. Pamoja na hayo, sababu za
kuomba marejeo si za msingi kwa kuwa waombaji uongozi na Kamati ya Uchaguzi ya
Yanga walipewa mwongozo wa kutosha kurekebisha upungufu uliojitokeza katika
mchakato wa uchaguzi wa kujaza nafasi za uongozi kwenye Klabu ya Yanga.
ii) Sara
Ramadhani hakutimiza masharti ya kuomba uongozi kwa mujibu wa Ibara ya 10(4) na
(5) ya Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF na kama ilivyoanishwa kwenye Fomu
namba 1 kwa kutojaza fomu na kutoambatanisha vithibitisho vya sifa za kugombea.
Kwa hiyo, Kamati ya Uchaguzi ya TFF inasisitiza uamuzi wake na kuitaka Kamati
ya Uchaguzi ya Yanga kuliondoa jina lake
katika orodha ya wagombea
uenyekikiti wa Klabu ya Yanga.
iii) Shaaban R.
Katwila na Ahmed Waziri Gao wameshindwa kutimiza masharti ya uombaji uongozi
kwa kutowasilisha vyeti halisi kwa ajili ya uhakiki kama
ilivyotakiwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) baada ya nakala za vyeti
vyao kubainika na NECTA kuwa vina utata. Kamati ya Uchaguzi ya TFF inaitaka
Kamati ya Uchaguzi ya Yanga kutekeleza uamuzi wa kuondoa majina yao kwenye orodha ya
wagombea uongozi wa Yanga.
iv) Ramadhan
Mzimba Kampira ameshindwa kutimiza masharti ya kugombea uongozi kama yalivyo
kwenye Ibara ya 10(5) ya Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF kwa
kutoambatanisha vithibitisho vya sifa za mgombea. Kwa hiyo, Kamati ya Uchaguzi
ya TFF inasisitiza uamuzi wake na kuitaka Kamati ya Uchaguzi ya Yanga kuondoa
jina lake katika orodha ya wagombea uongozi.
v) Kamati ya
Uchaguzi ya TFF inaridhia uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya Klabu ya Yanga
kuwaondoa wafuatao kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi:
(a) Ally Mayay
Tembele
(b) Abdallah
Sharia Ameir
(c) Jamal Hamisi
Kisongo
(d) Mohamed R
Mbaraka
vi) Wagombea
uongozi ambao hawakutajwa hapo juu na ambao walipitishwa na Kamati ya Uchaguzi
ya Yanga, wametimiza matakwa ya awali ya Kanuni za Uchaguzi za wanachama wa TFF
na hatua za mwisho za uhakiki wa vyeti vya elimu yao , zinaendelea.
Angetile Osiah
KATIBU
KAMATI YA UCHAGUZI TFF