TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Tukuyu stars
ni timu pekee yenye historia ya aina yake nchini Tanzania . Ilipanda daraja mwaka
1985, ikachukua ubingwa mwaka 1986,
ikashuka daraja mwaka 1987, ikapanda tena daraja mwaka 1988 na baada ya misimu
kadhaa ikashuka daraja na kupotea katika ramani ya mpira nchini. Hii ni historia ya pekee , lakini cha
kukumbukwa zaidi ilikuwa ni uwezo wa kusakata soka la nguvu, kasi, akili na
ubunifu wa wachezaji chini ya mwalimu
Athuman Juma ( marehemu).
Kutokana na
mwenendo na uwezo wa Tukuyu stars, timu hii ilivuta mashabiki wengi kila kona
ya nchi na Duniani. Hivyo wadau, wapenzi
na watu wengine walioguswa na kupotea kwa Tukuyu stars kwenye ramani ya soka
nchini wameanzisha mkakati wa kuifufua na kuirejesha Tukuyu stars kwenye ramani
ili tuendelee kupata ladha tuliyoikosa, yaani zile burudani za akina Selemani
Mathew, Karabi Mrisho, Stephen Mussa ( marehemu), Salum Kabunda Ninja
(marehemu), Ally Kimwaga, John Alex, Richard Lumumba, Aston Pardon na wengineo.
Hivyo lengo ni kuifufua na kurekebisha mfumo wa uendeshaji wa timu uwe wa
kisasa hasa kampuni ili iwe endelevu, shindani na inayojitegemea kiuchumi na
kimaamuzi. Kwa maana hiyo wadau, wapenzi na wengine wote wanaoguswa na
kutokuwepo kwa Tukuyu stars mnaalikwa kujumuika kwenye mpango huu.
Katika
kufikia malengo yaliyowekwa wadau wameanza utekelezaji wa mpango huu katika
ngazi mbalimbali ikihusisha wadau waliopo Dar
es salaam na wale waliopo Mbeya.
i)
Vikao vya wadau waishio Dar es
salaam vimeanza na vinaendelea kila ijumaa kuanzia saa
kumi na nusu jioni Kinondoni Mkwajuni, Katumba bar. Mada kuu ikiwa ni namna
bora ya kuifufua na kuirejesha Tukuyu stars.
ii)
Wadau wa Tukuyu stars waliopo Mbeya wanaendelea na vikao vya kufanikisha
siku rasmi ya kongamano la kufufuka kwa Tukuyu stars.
iii) Ili kuleta hamasa na kuibua vipaji vitakavyounda Tukuyu
stars ijayo ligi ndogo imeanzishwa Wilayani Rungwe mahali ilipozaliwa timu hii.
Ligi hii inategemea kukamilika yaani Fainali zake kuwa tarehe 04/08/2012
Siku ya
fainali yaani tarehe 04/08/2012 inatarajiwa kuwa siku ya kujadili na kufufuka rasmi kwa Tukuyu
stars, hii ni siku muhimu na inatarajiwa kuwa na matukio mengi na ya
kusisimua. Kutakuwa na michezo mitatu ya
utangulizi kabla ya mchezo wa fainali, pia kutakuwa na ngoma za asili maarufu kama Ing’oma. Michezo itakuwa kama
ifuatavyo:-
i)
Mechi ya awali ya vijana chini ya miaka 14 ( under 14) walioalikwa
wakishindana na wenyeji
ii)
Mechi ya vijana chini ya miaka 17 ( under 17) itafuatia, pia ikihusisha
timu waalikwa watakaoshindana na wenyeji.
iii) Baada
ya mechi hizo zitafuatia ngoma za asili
(Mang’oma)
iv) Itafuatia mechi ya kukata na shoka ya
wakongwe (veterans )waliochezea Tukuyu
stars na timu zingine waliopo Dar es salaam chini ya mwalimu Kennedy Mwaisabula
‘’mzazi’’ wakishindana na wakongwe
wenzao (veterans) waliopo Mbeya wakiongozwa na Jimmy Mored na Alex Mwambipile
v) Baada
ya mechi ya Veterans itafuatia fainali ya ligi inayoendelea, ili kumpata bingwa
wa mashindano yaliyoanza June.
Kilele cha
shughuli hii kitahitimishwa kwa kongamano kubwa la kuifufua rasmi Tukuyu stars,
mjadala huu utahusisha kuona namna bora ya kuendesha timu, na kama ni kampuni
basi uuzaji wa hisa utaanza siku hiyo kwa kuorodhesha majina ya wote wanaopenda
kununua hisa za kampuni na kujadili namna ya upatikanaji wa Bodi ya timu na
watendaji wa timu. Katika kongamano hili zitatolewa tuzo rasmi kwa waanzilishi
na viongozi wa Tukuyu stars, wanaotegemewa kupewa tuzo ni kama Ramnik Patel
Kaka (muasisi), mzee Kasyupa (katibu mkuu wa kwanza), mzee Malakasuka,
aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Mbeya Major
General (mstaafu) Rashid Nalihinga Makame , mzee Mwakasala na wale wote
waliojitoa kwa hali na mali kuifanya Tukuyu stars ing’are katika medani ya
soka.
Pia vitakabidhiwa vifaa vya awali kwa ajili ya kuanza rasmi
kambi ya timu ya Tukuyu stars.
Maandalizi
ya timu ya veterans waliopo Dar es salaam yanatarajia kuanza siku ya jumamosi
na kusimamiwa na mwalimu Kennedy Mwaisabula katika viwanja vya Harbours Pub
kurasini kuanzia saa mbili asubuhi.
Wachezaji wanaotarajiwa kucheza mechi hiyo na kuanza mazoezi ni:-
Godwin Aswile ‘’Mlimba’’
‘’Scania’’ ( Baba Subi), Seleman Mathew,Karabi
Mrisho,Salum
Kussi,Asanga Aswile, Mbwana Makata,Peter
Mwakibibi, Sekilojo Chambua, Nsajigwa Mwaisaka,Geofrey Amanyisye,Ezekiel ( Masatu),Shedrack
Nsajigwa Fusso, Christopher Michael, Lawrence
Mwalusako, John
Mwansasu, Deo Philip
Masanja, Michael
Mbaruku, Ally Kassimu, Nsangalufu
Joseph.
Kupitia taarifa hii tunawaalika wachezaji na wadau wote
wanaopenda kushiriki kwenye mazoezi na
kucheza mechi hii wafike jumamosi
asubuhi saa mbili katika viwanja vya
Harbours pub.
Vikao vya
mikakati ya kufufua Tukuyu stars vinaendelea kila ijumaa saa kumi na nusu jioni
kinondoni Mkwajuni Katumba bar hivyo wapenzi na wadau wote mnaalikwa ili tuweze kupanga kwa pamoja,
pia tujadili namna ya kusafiri kwenda Tukuyu Mbeya kwa ajili ya hiyo siku
rasmi.
Michezo
inaburudisha, inatoa ajira, inajenga undugu na zaidi ya hapo inawafanya
wanajamii wasahau tofauti zao na kuungana kusonga mbele katika maendeleo yao . Tunawaombeni wadau
wote wenye mapenzi mema na Tukuyu stars tuungane ili turudishe heshima ya miaka
ya 1980 wakati Tukuyu stars ikipambana
na Simba ya Dsm, Yanga ya Dsm, Pamba ya Mwanza, Ushirika ya Moshi, Mecco ya
Mbeya, Coastal Union ya Tanga, Nyota Nyekundu ya Dsm, Sigara ya Dsm, Pilsner ya
Dsm, Lipuli ya Iringa na timu nyingine. Tujumuike ili tuzalishe wachezaji
mahiri kama Justin Nicodemus Mtekele (
marehemu), Aston Pardon, Sekilojo Chambua, Hussein Zito, Stephen Mussa (
marehemu), Jabir Mohamed ( marehemu), Peter Mwakibibi na wengine
wengi.