Viingilio vya chini katika mashindano ya Kombe la Kagame yanayoanza Jumamosi (Julai 14 mwaka huu) vitakuwa sh. 5,000 kwa mechi za Yanga na Simba, na sh. 2,000 kwa mechi ambazo hazihusishi timu hizo. Yanga ni bingwa mtetezi wakati Simba ni makamu bingwa mtetezi.
Kwa upande wa mechi zinazohusisha Yanga na Simba viingilio vitakuwa kama ifuatavyo; viti vya bluu na kijani sh. 5,000, viti vya rangi ya chungwa sh. 7,000, viti vya VIP C sh. 10,000, viti vya VIP B sh. 15,000 na viti vya VIP A ni sh. 20,000.
Siku ambazo Simba na Yanga hazichezi, viingilio vitakuwa sh. 2,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani, sh. 5,000 kwa viti vya VIP C, sh. 10,000 kwa viti vya VIP B na sh. 15,000 kwa viti vya VIP A. Mshabiki akikata tiketi moja anaona mechi zote mbili; mechi ya saa 8 na ile ya saa 10.
Timu za El Salam Wau ya Sudan Kusini na Atletico ya Burundi zimewasili Dar es Salaam jana usiku (Julai 11 mwaka huu) tayari kwa mashindano hayo wakati nyingine zote zilizobaki kutoka nje zinawasili leo katika muda tofauti.