WAKATI mfungaji bora wa klabu bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati
‘Kombe la Kagame’ Yanga SC, Said
Bahanuzi ‘Spider Man’ akitua nchini Rwanda leo, mabingwa hao kesho watashuka katika
Uwanja wa Nyamirambo Kigali, Rwanda kuikabili Polisi ya huko katika mchezo wa
kujipima nguvu.
Bahanuzi hakuwemo katika msafara wa Yanga uliokwenda
nchini Rwanda katikati ya wiki iuliyopita kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo Paul
Kagame kwa ajili ya kuwapongeza kutokana na kutwaa ubingwa wa Kagame iyoutwaa
kwa mara ya pili mfululizo wiki mbili zilizopita, Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam kwa kuifunga Azam FC mabao 2-0, kutokana na kuwa na matatizo ya
kifamilia.
Akizungumza kwa simu kutoka Rwanda, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga Abdallah Binkleb alisema
kwamba, Bahanuzi aliwasili huko kutokea Dar es Salaam na kuungana na wenzake
ambapo kama kocha ataridhika na kiwango chake
huenda leo akacheza mechi yao
dhidi ya maafande.
Alisema timu yao ambayo jana ilianza vema mechi zake za kujipima nguvu nchini humo baada ya kuichapa Rayon
Sport mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Amahoro mjini Kigali, pamoja na ushindi huo
ilipoteza mabao mengi ya wazi baada ya washambuliaji wake kushindwa kutumia
vema nafasi za wazi walizotengeneza.
Binkleb alisema katika mchezo
wao huo na Rayon, mabao ya Yanga
yalipachikwa na Hamisi Kiiza katika dakika ya pili ya mchezo huo na Simon Msuva aliyefunga la pili katika dakika ya
12.
Akizungumzia mchezo wao wa kesho na Polisi, Binkleb alisema anaamini timu yao itatoka tena kifua mbele kwani
jana kocha wake mkuu, Mbelgiji Tom Saintfiet alifanyia kazi mapungufu
yaliyojitokeza juzi hivyo anaamini kitashuka kikosi bora zaidi.
Aliongeza kuwa, mchezo wa leo
utahitimisha ziara yao huko iliyoanza katikati ya wiki iliyopita abapo keshokutwa wanatarajiwa kurejea jijini Dar es Salaam keshokutwa kuendelea na maandalizi mengine ya
ligi kuu soka Tanzania Bara inayotarajiwa kuanza Septemba 15.
Pamoja na michezo hiyo, Yanga
ilipata kuzuru makumbusho ya Kimbari ambayo walizikwa wahanga waliofariki
katika mauaji yaliyotokea nchini humo mwaka 1994 kutokana na ugombi wa
kikabila.
Yanga pia ilipata fursa ya
kutembea Ikulu ya Rwanda na kuonana na Rais Kagame ambapo walizungumza maswala
mbalimbali ikiwemo mikakati ya kuendeleza uhusiano mzuri wa kimichezo baina
yao.
Katika ziara hiyo, Yanga
inaongozwa na Mwenyekiti Yussuf Manji, Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga na
Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini Mama Fatma Karume, Francis Kifukwe na Seif Ahmed
‘Magari’ pamoja na Wajumbe wa Kamati ya
Utendaji, Abdallah Bin-Kleb na Salum Rupia, huku viuongozi wa benchi la ufundi
ni kocha mkuu; Tom Saintfiet, Kocha Msaidizi Fred Felix Minziro, Kocha wa
makipa, Mfaume Athumani, Meneja Hafidh Saleh, Daktari, Sufiani Juma na Mtunza
vifaa Mahmoud Omary.
Kwa upande wa wachezaji ni
makipa: Yaw Berko, Ally Mustafa ‘Barthez’ na Said Mohamed. Mabeki Shadrack
Nsajigwa, Godfrey Taita, Juma Abdul, Oscar Joshua, Stefano Mwasyika, David
Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondan, Ibrahim Job, Ladisalus Mbogo;
viungo Athumani Iddi ‘Chuji’, Juma Seif ‘Kijiko’, Salum Telela, Simon Msuva,
Shamte Ally, Omega Seme, Idrisa Rashid, Nizar Khalfan, Haruna Niyonzima, Frank
Domayo, Rashid Gumbo, Nurdin Bakari na washambuliaji; Hamis Kiiza ‘Diego’,
Jerry Tegete na Didier Kavumbangu.