Kiiza katika mechi ya leo. (Picha na Saleh Ally wa Championi) |
Yanga ambao jana walitembelea Ikulu ya Rwanda, walipoalikwa na rais Paul Kagame kupeleka Kombe la Afrika Mashariki na Kati, ambalo tangu mwaka 2002 mfadhili wake mkuu na mlezi wake ni Rais Kagame, mabao yake yalitiwa kimiani na Hamisi Kiiza dakika ya pili na Simon Msuva dakika 12.
Katika mchezo huo, kikosi cha Yanga kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Nsajigwa Shadrack/Stefano Mwasyika, Oscar Joshua/Mbuyu Twite, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’/Frank Damayo, Simon Msuva, Haruna Niyonzima/Omega Seme, Didier Kavumbangu, Hamisi Kiiza/Jerry Tegete na Nizar Khalfan/Shamte Ally.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Abdallah Ahmad Bin Kleb ameiambia BIN ZUBEIRY kwa simu kutoka Kigali kwamba, timu yao ilicheza vema na kuwazidi kabisa uwezo wenyeji wao.
Alisema Yanga ilikuwa ina uwezo wa kufunga mabao zaidi, kama washambuliaji wake wangetumia vema nafasi zote walizotengeneza.
Bin Kleb alisema kwamba Yanga itashuka tena dimbani kumenyana na Polisi Jumapili na kwa mujibu wa ratiba ya awali, wanatakiwa kurejea Dar es Salaam Jumatatu.
Awali, Yanga ilikuwa icheze pia na mabingwa wengine wa zamani wa Kombe la Kagame, APR, lakini kutokana na timu hiyo kukabiliwa na mgogoro hivi sasa uliosababisha kufukuzwa kwa kocha Mholanzi, Ernest Brandy na nafasi yake kupewa kocha mzalendo kwa muda, imeshindwa kucheza.
Katika ziara hiyo, Yanga haijaambatana na mfungaji bora wa Kombe la Kagame, Said Bahanuzi ambaye amebaki Dar es Salaam kwa matatizo ya kifamilia. Yanga imekwenda Rwanda na msafara wa watu 42, wakiwemo wachezaji 28, Maofisa watano wa benchi la Ufundi na viongozi wanane.
Viongozi walio na timu Kigali ni Mwenyekiti, Yussuf Manji, Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga na Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini Mama Fatma Karume, Francis Kifukwe na Seif Ahmed ‘Magari’ sambamba na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji, Abdallah Bin-Kleb na Salum Rupia.
Benchi la ufundi ni kocha mkuu; Tom Saintfiet, Kocha Msaidizi Fred Felix Minziro, Kocha wa makipa, Mfaume Athumani, Meneja Hafidh Saleh, Daktari, Sufiani Juma na Mtunza vifaa Mahmoud Omary ‘Mpogolo’, wakati wachezaji ni makipa: Yaw Berko, Ally Mustafa ‘Barthez’ na Said Mohamed. Mabeki Shadrack Nsajigwa, Godfrey Taita, Juma Abdul, Oscar Joshua, Stefano Mwasyika, David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondan, Ibrahim Job, Ladisalus Mbogo; viungo Athumani Iddi ‘Chuji’, Juma Seif ‘Kijiko’, Salum Telela, Simon Msuva, Shamte Ally, Omega Seme, Idrisa Rashid, Nizar Khalfan, Haruna Niyonzima, Frank Domayo, Rashid Gumbo, Nurdin Bakari na washambuliaji; Hamis Kiiza ‘Diego’, Jerry Tegete na Didier Kavumbangu.
Yanga ilitwaa Kombe la Kagame kwa mara ya pili mfululizo wiki mbili zilizopita, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa kuifunga Azam FC mabao 2-0, ambayo yalitiwa kimiani na Hamisi Kiiza ‘Diego Milito’ na Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
Hiyo kwa ujumla ilikuwa mara ya tano mfululizo, Yanga inatwaa Kombe hilo, baada ya awali kuchukua mwaka jana, wakiifunga Simba katika fainali bao 1-0, Uwanja wa Taifa mfungaji Kenneth Asamoah ambaye ametemwa, ingawa siku hiyo Kiiza pia alifunga bao safi, ambalo refa alilikataa.
Yanga ilichukua kwa mara ya kwanza Kombe hilo, mwaka 1975 ikiifunga tena Simba katika fainali, mabao 2-0 wafungaji Sunday Manara ‘Computer’ na Gibson Sembuli (sasa marehemu) Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Ikachukua tena mwaka 1993, Uwanja wa Nakivubo, Kampala, Uganda kwa kuifunga SC Villa mabao 2-1, yaliyotiwa kimiani na Said Nassor Mwamba ‘Kizota’ (sasa marehemu) na Edibily Jonas Lunyamila.
Ilichukua tena mwaka 1999, ikiifunga tena SC Villa, Uwanja wa Nakivubo, kwa penalti 5-3, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 120, Yanga ikisawazisha bao kupitia kwa Lunyamila, baada ya Hassan Mubiru kutangulia kuifungia Villa, siku hiyo Manyika Peter akicheza penalti mbili za Waganda.
Aidha, kwa kutwaa Kombe hilo chini ya Mbelgiji huyo, Yanga imeendeleza rekodi yake ya kutwaa mataji ya michuano hiyo, chini ya makocha wa kigeni baada ya mwaka 1975 kuchukua chini ya Tambwe Leya aliyekuwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kabla ya kuchukua uraia wa Tanzania, (sasa marehemu), 1993 chini ya Nzoyisaba Tauzany aliyekuwa raia wa Burundi kabla ya kuchukua uraia wa Tanzania, mwaka 1999 chini ya Raoul Shungu wa DRC na mwaka jana chini ya Mganda, Sam Timbe.
HABARI: http://bongostaz.blogspot.com