MABINGWA wa
soka Afrika Mashariki na Kati, Yanga ya jijini Dar es Salaam leo inatarajiwa
kushuka kwenye dimba la CCM Kirumba jijini Mwanza kuwavaa wenyeji Toto African
katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom.
Yanga
itashuka uwanjani ikiwa bado na maumivu ya kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Kagera
Sugar ya Kagera mjini Bukoba Jumatatu.
Katibu Mkuu
wa Yanga, Lawrance Mwalusako, alisema jijini Dar es Salaam jana kwamba, baada ya kipigo
cha Kagera, wamefanyia kazi upungufu uliojitokeza na anaamini watashinda leo.
Alisema
zaidi ya kuwaweka sawa wachezaji kwa ajili ya mchezo huo, pia wamewajenga
kisaikolojia ili waweze kusahau ya Kagera na kuelekeza nguvu katika michezo
mingine ya ligi hiyo.
“Mchezo ni
mchezo lazima kuwepo na upinzani, hivyo nasema utakuwa ni mgumu…kikubwa ni kuwa
tumejipanga katika kila idara kuhakikisha tunaondoka na pointi tatu,” alisema.
Katika
mchezo wa leo, Yanga itawakosa nyota wake muhimu wakiwemo beki Kelvin Yondani
pamoja na Said Bahanuzi ambao ni majeruhi.
Yanga hivi
sasa inakamata nafasi ya nane katika msimamo wa ligi, ikiwa na pointi 8 baada
ya kushuka dimbani mara sita.