Ligi Kuu ya
Vodacom (VPL) inaingia raundi ya pili kesho (Agosti 24 mwaka huu) kwa timu zote
14 kuwa viwanjani huku macho na masikio ya washabiki wengi yakielekezwa kwenye
mechi kati ya Yanga na Coastal Union.
Mechi hiyo
itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.30 jioni kwa kiingilio
cha sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000. Mwamuzi Martin Saanya wa
Morogoro ndiye atakayepuliza filimbi wakati Kamishna atakuwa Omari Walii kutoka
Arusha.
Mtibwa Sugar
itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani
Morogoro wakati Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora utakuwa mwenyeji wa
pambano kati ya wenyeji Rhino Rangers na Azam.
Vumbi
lingine litatimka kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani wakati
maafande wa JKT Ruvu watakapokwaruzana na wenzao wa Tanzania Prisons kutoka
Mbeya. Mbeya City na Ruvu Shooting zitacheza kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya
Sokoine jijini Mbeya.
Jiji la
Tanga litakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Mgambo Shooting na Ashanti United
itakayochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani. Oljoro JKT itakuwa mwenyeji wa Simba
kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha.