NYOTA wa kimataifa wa Simba Amisi Tambwe na Gilbert Kaze kutoka Burundi wanatarajiwa
kutambulishwa rasmi jumapili hii kupitia mchezo wa kirafiki baina ya Simba na
Mafunzo inayoshiriki ligi kuu ya Zanzibar utakaopigwa kwenye uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam.
Huo utakuwa mchezo wa kwanza kwa wachezaji hao ambao pia
wanakipiga katika timu ya Taifa ya Burundi ‘Intamba Murugamba’kukichezea kikosi
cha Simba jijini dar es Salaam tangu kujiunga nayo kwa ajili ya kuichezea
kwenye msimu wa ligi wa 2013/2014.
Katibu Mkuu wa Simba Evodius Mtawala ameiambia SPORTS LADY BLOG kwamba mchezo huo
ni maalum kwa ajili ya kuwatambulisha wachezaji hao baada ya kushindwa kufanya
hivyo katika tamasha la Simba Day.
Alisema mchezo huo ni zaidi ya mechi ya kirafiki kwani
utasaidia kukiweka sawa kwa namna moja ama nyingine kikosi cha Simba ambacho
kinaendelea na michezo yake ya Ligi Kuu soka Tanzania Bara iliyoanza mkutimua
vumbi juzi iliyopita.
Hata hivyo wachezaji hao walishindwa kuichezea Simba kwa
sababu ya kutokuwa na hati za uhamisho wa Kimataifa (ITC) kabla ya mwenyekiti
wa Simba Ismail Aden Rage kufunga safari hadi Burundi na juzi kurejea nazo na
hivyo kufanya wachezaji hao kuwa tayari kuichezea timu yao katika michezo itakayofuata.
Mtawala aliongeza kuwa kikosi cha Simba ambacho kipo njiani
kwa ajili ya kuelea mjini Arusha tayari kwa mchezo wake wa ligi kuu bara dhidi
ya wenyeji JKT Oljoro utakaopigwa keshokutwa kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid
mjini Arusha.
Mchezo baina ya Simba na Oljoro utakuwa wa pili ambapo katika mchezo wa awali wa ligi hiyo ililazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Rhino ya Tabora, mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.