NCHUNGA
MGOMBEA nafasi ya uenyekiti katika klabu ya Yanga, Llyod Nchunga ameishauri kamati ya uchaguzi ya klabu hiyo kuheshimu katika kwa kuendesha uchaguzi huo katika mazingira ya wazi ili kuwapata washindi na washindwa kihalali.
Nchunga aliyasema hayo leo na kutolea mfano wa chaguzi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwani kinyume na hapo, itakuwa ni kutowatendea haki wagombea na wanachama kwa ujumla.
“Kupiga kura ni jambo la siri ya kila mmoja, lakini tunataka uwazi katika zoezi zima ikiwemo masanduku ya kupigia yawe na uwazi na hata kura zihesabiwe kwa uwazi ili kuepusha hali yoyote ya upangaji matokeo.
Katika hatua nyingine, Nchunga amewaomba radhi wanachama wote ambao hajawafikia katika kampeni yake ya kuomba kura na kusema yupo pamoja nao na watamkia zaidi katika ukumbi hapo kesho wakati wa kujieleza.
Kwa upande wa sera za Nchunga, mbali ya kuyaunganisha matawi na kuyajengea nguvu zaidi ya kiuchumi, pia yatakuwa yakisimamia timu kwa utaratibu bora huku yakipata sehemu ya mapato ya milangoni.
Mipango mingine ya Nchunga, ni kupiga vita makundi, kuanzisha Saccos ambayo baadaye itakuwa benki na kuwasihi wanachama wa Yanga kumpatia kura zao.
Mbali ya Nchunga, nafasi hiyo inawaniwa na Mbaraka Igangula, Edger Chibura na Abeid Abeid ambao kesho watachuana vikali katika ukumbi wa PTA uliopo katika viwanja vya maonyesho ya Sabasaba.