VODACOM YADHAMINI TAMASHA LA MTIKISIKO MJINI IRINGA NA MBEYA

WANENGUAJI WA KIUME WA TWANGA PEPETA AMBAYO ITATOA BURUDANI KATIKA TAMASHA HILO
TAMASHA la Mtikisiko linalotarajiwa kufanyika katika mikoa ya Iringa na Mbeya, litafanyika Novemba 6 kwa Mbeya, Uwanja wa Sokoine, wakati Iringa litafanyika Novemba 13, huku kampuni ya Simu za Mikononi ya Vodacom Tanzanzania, ikidhamini kwa Sh Milioni 22.
Tamasha hilo limeandaliwa kwa mara ya nne mwaka huu na Ibony Entertainment ya mkoani Iringa na kupewa jina la 'Bata Mrefu', kwa nia ya kuwakutanisha viijana na wapenzi wa mambo ya burudani, huku pia likiwakutanisha vijana na kujadiliana vitu vinavyowakabili.
Mwakilishi wa tamasha hilo, kutoka Ibony, Leah Mbeyale, alisema kwamba tamasha hilo litashirikisha wasanii mbalimbali, wakiongozwa na bendi inayotamba kwa sasa, The African Stars Twanga Pepeta.
Pia kutakuwapo na michezo mingine, ikiwamo Pool table na masumbwi, huku wakiamini kwamba onyesho la mikoa miwili, litatumika kama sehemu ya kufurahia burudani za tamasha hilo lenye mguso mkubwa kwa mashabiki wa burudani.
Kwa mujibu wa Leah, tamasha hilo la Mtikisiko, limepiga hatua kubwa baada ya kufanikiwa kuongeza mikoa ya kufanya tukio hilo na kuchangia kwa kiasi kikubwa kuongeza hamasa kwa wote watakaohudhuria.
"Tangu lianzishwe tamasha hili, limekuwa na mguso mkubwa mkoani Iringa, kitu kilichotuongezea hamasa na hamu ya kuona mikoa mingine wanapata fursa ya kusherehekea tukio hilo lenye dira na mguso kwa wadau wote wa Mbeya na Iringa.
"Wadau waje kwa wingi, kwani kiingilio ni cha chini kabisa, Sh 5,000 huku ulinzi ukiwa wa kutosha wakati wote wa tamasha hilo, Novemba 6 huko Mbeya na hata Iringa pia kila kitu kitawekwa sawa ili kuwapatia kitu kizuri wadau wa mambo ya burudani kutoka kwetu," alisema Leah.
Naye Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania, Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Jackson Kiswaga, alifurahia kudhamini tamasha hilo, huku akisema kwamba litakuwa maalumu kwa wadau wao, kuifahamu vyema Vodacom na kusherehekea pia miaka 10, tangu kuanzishwa kwake.

Post a Comment

Previous Post Next Post