Baadhi ya wadau wa Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu kwenye Ukumbi wa BASATA wakinyoosha mikono juu kama ishara ya kula kiapo cha kupambana na rushwa, uvivu na kutokuwajibika.Kiapo hicho kiliongozwa na Msanii maarufu wa muziki wa falsafa,Vitalii Maembe aka Sumu ya Teja.
Mkongwe wa dansi nchini Mzee Kassim Mapili (kulia) akimpa makabrasha msanii Vitali Maembe ili ayatumie kwenye mapambano dhidi ya dhuluma kwa wasanii na jamii kwa ujumla.
Nyomi kwenye Jukwaa la Sanaa.Kwa sasa linakua kwa kasi na kuvuta watu kutoka pande mbalimbali za jiji la Dar es Salaam na vitongoji vyake.
Na Mwandishi Wetu
Wadau wa Jukwaa la Sanaa mapema wiki hii wamekula kiapo cha kupambana na rushwa pia dhuruma nchini huku wito ukitolewa kwa wasanii kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya matatizo hayo ambayo kwa sasa yanatajwa kuwa kikwazo katika kuleta maendeleo ya mtanzania.
Akiwasilisha mada kwenye Jukwaa hilo linalofanyika kila Jumatatu kwenye Ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) Juu ya Wasanii na Ukombozi wa Jamii,Msanii Vitali Maembe maarufu kama Sumu ya Teja alisema kwamba,sanaa ni chombo kilichoshushwa na Mungu kwa ajili ya kuikomboa jamii dhidi ya makucha mbalimbali ikiwemo rushwa na ufisadi hivyo wadau wa sanaa hawana budi kuitumia katika kuikomboa jamii.
“Kama kuna watu watapewa adhabu na Mungu kwa kutotimiza wajibu wao ipasavyo basi ni wasanii.Mungu ametupa sanaa ambacho ni chombo chenye nguvu katika kuikomboa jamii lakini badala ya kuitumia kwa kazi hiyo,tumeigeuza chombo cha starehe, kujizolea umaarufu na kupatia wanawake” alilalamika Vitali Maembe.
Aliongeza kwamba,yeye katika kazi zake za sanaa hataacha kuimba ukweli na matatizo halisi yanayoigusa jamii ingawa kuna watu wanachukizwa na msimamo huo na kwamba anaamini ameingia kwenye tasnia hii kuikomboa jamii na wajibu wa suala hilo ni wa msanii yeyote.
“Kuna watu wanachukizwa sana na mimi kuimba ukweli na matatizo yanayoikumba jamii,mimi sitaacha kufanya hivyo hata nikitishiwa na nyimbo zangu kuzuiwa kupigwa.Sanaa imegeuzwa chombo cha starehe na kutukuza anasa wakati jamii inateketea” aliongea kwa uchungu Maembe huku akiimba nyimbo zenye ujumbe mzito kama Afrika shilingi tano,sumu ya teja na nyingine nyingi.
Katika kuhakikisha sanaa inatumika kupambana na rushwa,Vitali Maembe ameanza kampeni ya Chanjo dhidi ya rushwa, uvivu na kutowajibika ambayo kwa sasa imejikita mashuleni ambapo amekuwa akizunguka mikoa mbalimbali na kuhamasisha wanafunzi kujiepusha na vitendo hivyo ambayo vinalirudisha nyuma taifa.
Aidha,Maembe akiwa amewaomba wadau wa Jukwaa la Sanaa kunyosha mikono yao juu, aliwaongoza kutamka ahadi za Mwana TANU dhidi ya rushwa ambazo zilikuwa ni maarufu wakati Baba wa Taifa hayati Julius Kambarage Nyerere anaasisi azimio la Arusha mwaka 1967 ambapo pamoja mambo mengine lililenga kupinga dhuruma na rushwa ndani ya jamii.
Sambamba na Vitali Maembe ambaye alikonga vilivyo mioyo ya wadau wa Jukwaa, warembo wanaowania taji la Miss Utalii wanaotazamiwa kupanda jukwaani Jumamosi ya wiki hii walitoa burudani ya ngoma mbalimbali za asili na kuwa kivutio kwa wadau hao zaidi ya 200 waliohudhuria wiki hii.