SIMBA YAMUUZA BANKA YANGA KWA MILIONI 150



KLABU ya soka ya Simba imesema haitamuuza mchezaji yeyote chini ya dola za Kimarekani 100,000 (sawa na shilingi mil. 150 za Kitanzania).

Kutokana na hilo, ina maana kuwa Yanga wanaomtaka kiungo wa Simba, Mohammed Banka (Pichani)watatakiwa kulipa kiasi hicho cha fedha ili wampate.

Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage alisema kwamba kuanzia sasa hawatouza mchezaji wao yeyote kwa dau la chini ya dola 100,000, huku akiweka wazi kwamba wakati wa kusajili wachezaji kwa dola 10,000 umepita.

Pamoja na hilo, Rage alisema mpaka sasa klabu yake haijamtema mchezaji yeyote kutokana na kuwa bado wana mikataba, isipokuwa Mkenya George Owinio na Rashid Gumbo.

Yanga inadaiwa kuwa ipo katika mazungumzo na Banka, ambaye anaonekana kuchoshwa na Simba aliyoichezea tangu mwaka 2007.

Banka aliyejiunga Simba akitokea Yanga, hata hivyo bado ana mkataba wa mwaka mmoja.

Awali Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Seif Ahmed, aliwahi kusema kuwa hawako tayari kumnunua Banka na wenzake Mussa Mgosi, Kelvin Yondan na Juma Kaseja ambao kulikuwa na taarifa kuwa wataachwa, bali watakuwa tayari kuwachukua kama wachezaji huru.

Banka na wenzake waliingia katika mgogoro na viongozi wao baada ya Simba kukosa ubingwa wa Ligi Kuu bara msimu wa 2010/2011 licha ya kuongoza kwa pointi sita zikiwa zimebaki mechi tatu.

Kufuatia msigano huo zilikuwepo fununu za wachezaji hao kutaka kutemwa na Simba kabla ya kuibuka taarifa kuwa, Banka, Mgosi na Kaseja wana mpango wa kujiunga na Yanga.

Post a Comment

Previous Post Next Post