Mchezaji wa timu ya Mkoa wa Singida (Kindai Shooting Stars), Nassoro Issa (19) amefariki dunia leo saa 9 alasiri akiwa mazoezini kwenye uwanja wa Shule ya Sekondari Mwenge, mjini Singida.
Issa ambaye alikuwa mchezaji wa timu ya Aston Villa ya mjini humo alijisikia vibaya wakati akiwa mazoezini na kumuomba kocha wa Kindai Shooting Stars, Abdallah Msamba apumzike. Kocha huyo alimruhusu akapumzike chini ya mti nje ya uwanja.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Singida (SIREFA), Hussein Mwamba, Issa ambaye aliuwakilisha mkoa huo kwenye michuano ya Copa Coca Cola mwaka 2009 aliomba apewe maji ya kunywa.
Baada ya kupewa maji, alikunywa na kujipumzisha. Baadaye daktari wa Kindai Shooting Stars alikwenda kumuangalia ili kujua hali yake.
Hata hivyo baada ya kujaribu kumuinua aligundua kuwa ameshafariki dunia. Mwili wa marehemu ulipelekwa hospitali ya mkoa na baadaye nyumbani kwa baba yake mjini humo. Mazishi yalitarajiwa kufanyika leo au kesho.
TFF imepokea kwa masikitiko makubwa msiba huo na kutuma salamu za rambirambi SIREFA, hasa ikizingatiwa kuwa mchezaji huyo alikuwa bado kijana hivyo kuwa na fursa pana ya kutoa mchango katika maendeleo ya mpira wa miguu nchini, hasa kupitia Mkoa wake wa Singida. Mungu aiweke roho ya marehemu Nassoro Issa mahali pema peponi.
Amina.
Boniface Wambura
Ofisa Habari TFF