CHAKA KHAN YUPO TAYARI KUWAPA RAHA JUMAMOSI


MWANAMUZIKI nyota kutoka Marekani, ambaye pia ni gwiji wa miondoko ya soul, Chaka Khan, ameahidi kutoa burudani ya aina yake katika hafla ya Club E itakayofanyika katika Hoteli ya Blue Pearl, Ubungo Plaza, jijini Dar es Salaam keshokutwa.
Chaka Khan, ambaye aliwahi kupata tuzo ijulikanayo kama ‘BET Lifetime Achievement’ mwaka 2006, aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana, wakati wa ziara yake kwenye Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC), Barabara ya Nyerere.
“Niko tayari kwa onyesho hili. Huwa niko tayari kila mara,” alisema gwiji huyo wa miziki ya zamani.
Wakati wa ziara yake kiwandani hapo, msanii huyo alipiga picha za pamoja na wafanyakazi wa TCC na baadaye kupewa maelezo kuhusu shughuli mbalimbali za kampuni hiyo.
Katika mahojiano yake na waandishi wa habari, Chaka Khan alisema analeta Tanzania ujumbe wa amani, upendo na uponyaji.
“Huo ndio ujumbe wangu kwa Watanzania,” alisema msanii huyo mwenye miaka 58, aliyewasili nchini Jumatatu mchana.
Baadhi ya nyimbo za Chaka Khan zilizovuma zaidi miaka ya nyuma ni pamoja na ‘Tell Me Something Good’, ‘Sweet Thing’, ‘Ain't Nobody’, ‘I'm Every Woman’, ‘I Feel for You’ na ‘Through the Fire’.
Club E huandaa shughuli mbalimbali za burudani kila mwaka kwa wanachama wake, kama mojawapo ya njia ya kuwakutanisha, kuburudika pamoja na kuwashukuru.

Post a Comment

Previous Post Next Post