NDANI YA SAA 24:RAGE AINGIA MSITUNI NA KUZILETA ITC ZA HAMIS TAMBWE NA GILBERT KAZE

 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
 MWENYEKITI wa Simba, Mhe; Ismail Aden Rage, leo mchana amefanikisha upatikanaji wa Hati za Uhamisho wa Kimataifa (ITC), kwa wachezaji wawili wa klabu hiyo kutoka nchini Burundi -Amissi Tambwe na Gilbert Kaze. 
Wachezaji hao wawili ambao pia ni tegemeo la timu ya soka ya taifa ya Burundi (Intamba Murugamba), hawakucheza katika mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania iliyochezwa jana kutokana na kutokamlika kwa uhamisho huo, jambo lililoleta usumbufu mkubwa kwa benchi la ufundi, wachezaji wenyewe, uongozi na wapenzi na washabiki wa  klabu. 
Rage aliondoka jijini Dar es Salaam jana usiku na imechukua chini ya saa 24 kuweka kufanikisha suala hilo. Katika taarifa yake kwa wana Simba, Mbunge huyo wa Tabora Mjini alisema amelazimika kuingilia kati suala hilo kwa sababu lilihusu baadhi ya taratibu muhimu za Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na ukweli kwamba viongozi wa Vitalo, klabu waliyotoka wachezaji hao hawakuwa mjni na hivyo kuchelewa kwao kungeigharimu Simba. 
"Kila walipokuwa wakipigiwa simu kwa takribani siku tatu mfululizo walikuwa wakisema kwamba wako milimani. Sasa hawa watu wa Burundi wakikwambia wako miliman wanamaanisha wameenda kijijini kwao. Kuongea kwa simu pekee kusingetosha na ndiyo Kamati ya Utendaji ya Simba iliomba niende mwenyewe Burundi ili suala hili liishe," alisema. 
Hii ni mara ya pili kwa Rage, ambaye ana uzoefu wa kuongoza soka kwa zaidi ya miongo mitatu, kuingilia kati suala la uhamisho wa wachezaji wa kimataifa. Miaka miwili iliyopita, Mwenyekiti huyo alilazimika pia kusafiri kwenda nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kushughulikia uhamisho wa mchezaji Gervais Kago ambao nao ulikuwa na matatizo. 
Kutokana na kupatikana kwa ITC hizo, Kaze na Tambwe sasa wataruhusiwa kucheza katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya JKT OIljoro ya Arusha iliyopangwa kufanyika Jumatano ijayo mjini Arusha. Klabu ya Simba tayari imewakatia wachezaji hao vibali vya kufanya kazi hapa nchini. 
Wachezaji wengine wa kigeni wa Simba, Joeph Owino na Abel Dhaira, walicheza katika mechi ya jana kutokana na kukamilisha taratibu zote za uhamisho na kuwa na vibali vya kufanya kazi hapa nchini.
 
Imetolea na
 
Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
Simba SC
 

Post a Comment

Previous Post Next Post