KATIKA shamrashamra za kutwaa Kombe la Kagame, uongozi wa Klabu ya Yanga ukishirikiana na mwanamuziki nyota wa kike, Judith Wambura ‘Lady Jaydee au Jide’ leo wameandaa tafrija fupi ya chakula cha jioni katika mgahawa wa Nyumbani Lounge huku wadau wakiwachangia sh milioni 40.
Mbali ya wadau hao waliokunwa na ushindi huo kuchanga fedha hizo, pia uongozi utawaongezea ‘wapiganaji’ hao asilimia 80 ya mapato yaliyopatikana katika mechi ya fainali iliyopigwa Jumapili iliyopita Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Yanga, Mwesigwa Celestine, alisema tafrija hiyo ni kwa ajili ya kuwapongeza wachezaji baada ya kutwaa Kombe la Kagame.
Alisema mbali na tafrija hiyo, pia wachezaji wapo katika mapumziko mafupi na wanatarajiwa kurejea kambini Julai 20.
Alisema ushindi walioupata ni uthibitisho tosha kwamba wanaweza, japokuwa walifungiwa miaka mitatu na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).
Akizungumzia kuhusu motisha huo, alisema wadau mbalimbali wa soka nchini wamezawadia wachezaji sh milioni 40 na wao kama uongozi umepanga kuwapa asilimia 80 ya mgawo wao watakaopata katika mechi ya fainali.
Alisema kuwa fedha hizo watapatiwa wachezaji pamoja na benchi la ufundi, ikiwa ni kutambua mchango wao katika mashindano hayo kwani wamefanya kazi kubwa.
Katika mechi ya fainali Jumapili, Yanga ilibuka mshindi baada ya kuwafunga mahasimu wao Simba bao 1- 0 lililofungwa na Keneth Asamoah.
Katika hatua nyingine, Mwesigwa alikanusha taarifa zilizotolewa kuwa, beki wao, Nadir Haroub ‘Canavaro’, amechukuliwa na El Mereikh ya Sudan.
Mwesigwa alisema, anashangazwa na taarifa hizo na kwamba hazina ukweli, kutokana na wao kutopata tamko lolote kutoka kwa El Merreikh.