Shule ya Sekondari ya Makongo, jana imefuzu kucheza robo fainali ya michuano inayoendelea ya Airtel Rising Stars baada ya kuishinda shule ya Mpijimagohe sekondari kwa 4-0 kwenye mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa shule ya Makongo. Kwenye mechi ya ufunguzi, Makongo sekondari ilishinda kwa 5-1 dhidi ya shule ya sekondari ya Twiga. Michuano hiyo imedhaminiwa na kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania kwa kushirikiana na klabu ya Manchester United ya Uingereza.
Kwenye mchezo wa jana ambao tangu dakika ya mwanzo Makongo walionyesha hali ya ushindi ambapo washumbuliaji wa Makongo waliindamana lango la wapinzania wao kama nyuki huku wakikosa magoli ya wazi katika ya dakika ya 3, 7 na 11 ya mchezo. Hata hivyo, katika dakika ya kumi na sita, Omary Mtego aliwanyanyua mashabiki lukuki wa Makongo waliokuwa wakishangilia timu yao , baada ya kupata pasi murua kutoka kwa Daniel Stephen na kumchambua vema kipa wa Mpijimagohe na kuandika bao la kwanza. Baada ya bao hilo, Makongo walizindizwa mashambuli na kunamo dakika ya 22, Mohammed Kabeta iliongeza bao la pili baada ya kuunganisha krosi safi kutoka kwa Suleiam Mbovu, ambaye kwa mechi ya jana alikuwa ni mwiba mkali kwa mabeki wa Mpijimagohe. Baada ya bao, Mpijimagohe walifanya mabadiliko ambapo Issa Salum alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Christian Elias. Kwenye dakika ya 32, Suleiman Mbovu aliongeza bao la tatu kwa njia ya penati baada mshambuliaji Daniel Stephen kufanyiwa madhambi kwenye eneo la hatari na mwamuzi kuamuru penati ipingwe. Hadi timu zinakwenda mapumziko, Makongo walikuwa kifua mbele kwa mabao 3-0.
Kwenye mwanzo wa kipindi cha pili, Mpijimagohe walifanya tena mabadiliko ambapo Emmanuel Shauri alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Bonaface Mwinje na Ibrahim Ramadhan akitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Juma Haruna. Hata hivyo, mabadiliko hayo hayakufanya Makongo kuacha sherehe za magoli kwani mnamo dakika ya 54, Suleiman Mbovu aliifungia tena bao la nne kwa timu yake na la pili kwake mwenyewe. Baada ya bao hilo , Makongo walifanya mabadiliko kadhaa ambapo Daniel Stephen alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Hamed Ismail, Zuberi Mulindwa aliingia kuchukua nafasi ya Abubakari Katundu na Seleman Mbovu alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Hija Isaac. Baada ya mabadiliko hayo, Mpijimagohe ndio walianza kuonyesha uhai kwa kumiliki sehemu kubwa ya mchezo lakini mabeki wa Makongo walisimama imara kuokoa hatari. Mpaka dakika ya mwisho ya mchezo Mkongo ndio walitoka kifua mbele kwa 4-0.
Kwenye mechi ya awali ambayo pia ilichezwa kwenye uwanja huo, Shule ya Sekondari ya Goba iliifunga Twiga sekondari magoli 3-2. Kwenye mechi ya ufunguzi, Goba pia ilishinda Mpijimagohe kwa mabao 2-0.
Kwenye Kanda ya Temeke ambapo mechi zake zinachezwa kwenye uwanja wa Shule ya sekondari ya Kurasini, Jitegemee sekondari ilishinda 1-0 dhidi ya Mbande na Temeke sekondari ilitoshana nguvu na Kibugumo kwa kwenda sare ya bao 1-1. Kwenye Kanda ya Ilala ambapo mechi zake zinachezwa kwenye shule ya sekondari ya Airwing, Azania sekondari ilishinda 4-0 dhidi ya Misitu na Kinyerezi kwenda sare ya 1-1 dhidi ya Msogolo sekondari.
Michuano hiyo jana ilifunguliwa Mkoani Morogoro ambapo kwenye uwanja wa Morogoro Sekondari, Morongoro sekondari iliifunga shule ya sekondari ya Uwanja wa Taifa 3-2 na Shule ya Mwembesongo kuishinda Kihonda 3-1.
Mechi hizo zitaendelea leo Jumapili ambapo katika kanda ya Kinondoni kwenye uwanja wa Shule ya sekondari ya Makongo, Mpijimagohe atacheza na Twiga sekondari na Makongo akicheza na Goba sekondari. Kwenye Kanda ya Tekeme ambapo mechi zinachezwa kwenye uwanja wa sekondari wa Kurasini, Jitengemee atacheza na Temeke sekondari na Mbande kucheza na Kibugumo. Kanda ya Ilala kwenye uwanja wa shule ya Airwing, Azania sekondari atacheza na Kinyerezi na Misitu kucheza na Msogolo.