Timu ya Taifa ya Shelisheli imewasili leo mchana (Julai 22 mwaka huu) jijini
Arusha ikitokea Nairobi, Kenya kwa ajili ya mechi mbili za kirafiki dhidi ya
timu ya Taifa ya Tanzania ya vijana wenye umri chini ya miaka 23 (U23).
Mechi hizo zitachezwa Julai 27 na 30 mwaka huu kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya
Sheikh Amri Abeid Kaluta, jijini Arusha. Timu hiyo imefikia kwenye hoteli ya ya
Markelly’s.
Shelisheli imewasili na wachezaji 24 na viongozi sita akiwemo mchezaji wa
kulipwa
Kevin Betsy. U23 inaendelea na mazoezi Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es
Salaam chini ya Kocha Jamhuri Kihwelo na inatarajia kuondoka Julai 25 mwaka huu
kwenda Arusha tayari kwa mchezo huo.
Pia Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen amewajumuisha kwenye kikosi cha U23
wachezaji Juma Seif Kijiko wa Yanga, Haruna Moshi wa Simba na Gaudence Mwaikimba
ambaye msimu huu ameombwa usajili Moro United.
Lengo la Poulsen ni kuangalia kiwango cha wachezaji hao ili kuona kama anaweza
kuwajumuisha kwenye kikosi cha Taifa Stars ambacho Agosti 10 mwaka huu kitacheza
na Palestina katika mechi ya kirafiki itakayofanyika jijini Ramallah. Poulsen
atataja kikosi hicho Julai 31 mwaka huu jijini Arusha baada ya mechi hizo mbili.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)