TIMU ya Taifa ya soka ya Wanawake ‘Twiga Stars’ imesema ushiriki wao wa michuano ya Shirikisho la Vyama vya Soka Kusini mwa Afrika (COSAFA) iliyomalizika hivi karibuni, Hararre Zimbabwe na wao kutwaa nafasi ya tatu imefunza mengi kwenye.
Akizungumza jijini Dar es Salaam mara baada ya kuwasili, Kocha mkuu wa timu hiyo Charles Boniface Mkwasa alisema kuwa mafunzo hayo yatawasaidia kwenye mashindano ya All Africa Games yanayotarajia kufanyika Septemba 3 hadi 18 huko Maputo, Msumbiji.
Alisema kikosi chake cha sasa huwezi kukilinganisha na kile cha zamani kwa kuwa wachezaji wamekomaa katika kila idara hali iliyopelekea kutimiza wajibu wao na hivyo kufanya vema licha ya kutobahatika kutwaa Ubingwa.
“Tumepata uzoefu mkubwa wa kushiriki mashindano makubwa kama hayo hivyo ni matarajio yetu tutafanya vizuri kwenye mashindano ya Afrika kwa sababu wachezaji wamepata uzoefu na mafunzo ya kutosha hivyo kwa sasa ni kuendelea na mazoezi sambamba na kurekebisha kasoro ndogo ndogo,”Aliongeza.
Mkwasa alisema kuwa baada ya wiki mbili timu inatarajia kuingia kambini kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya ‘All Africa Games’ huku akisema wachezaji wanatakiwa wapate mazoezi ya kujenga miili yao ambapo amesema wataliomba Shirikisho la soka Tanzania (TFF), ili liweze kuwapatia nafasi ya kufanya mazoezi ya viungo.
Wachezaji hao waliorejea jana ni pamoja na , Asha Rashid (Mburahati Queens), Neema Jacob (SimbaQueens), Sophia Mwasikili (Sayari), Fadhila Hamad (Uzuri),Mwanahamisi Omar (Mburahati Queens),Fatuma Omar (Sayari), Fatuma Swalehe ‘Kitu Nini’ (Simba Queens), Maimuna Mkane (JKT),Pulkelia Charaji (Sayari), Fatuma Makusanya (Simba Queens), Mwanaidi Tamba(Mburahati Queens), Fridiana Daudi (JKT), Fatuma Salum (Mburahati Queens), Mwajuma Abdillah (Tanzanite), Mariam Fakil (Tanzanite), Mwasiti Selemani (Tanzanite),Aziza Lugendo (Mburahati Queens), Suzana Komba (TMK) na Rukia Hamisi (Evergreen),