CHUJI AREJEA TENA YANGA


Na Dina Ismail

HABARI ndiyo hiyo, mabingwa wa ligi kuu soka Tanzania Bara, Yanga imesajili kiungo wa zamani wa Simba Athuman Idd ‘Chuji’ kwa ajili ya kuitumikia timu hiyo katika mzunguko wa pili wa ligi kuu soka Tanzania Bara na michuano ya kimataifa, imefahamika.
Habari za kuaminika kutoka Yanga zinasema kwamba Chuji alimwaga wino wa kuichezea timu hiyo kwa miaka miwili baada ya kukamilisha mazungumzo kati ya mchezaji huyo na viongozi wa kamati ya usajili.
“Ni kweli Chuji tumemsainisha Chuji mkataba wa miaka miwili baada ya kukamilka kwa mazungumzo, hivyo Chuji ni mmoja kati ya wachezaji watakoavaa uzi wa kijani na njano katika mzungo wa pili wa ligi kuu bara na michuano ya kimataifa,”Alisema kiongozi mmoja wa Yanga ambaye hakupenda kutajwa jina lake.
Hata hivyo, huenda klabu hiyo ikaingia tena katika mgogoro wa kumgombea klabu hiyo na mahasimu wao nchini, Simba ambayo mwaka huu ilimsainisha mkataba wa miaka kabla ya kumpeleka kwa mkopo katika klabu ya Villa Squad.
Hali ya kuuzwa kwa mkopo Villa Squad haikumridhisha Chuji ambaye aligoma kuichezea timu hiyo na kudai kuwa yuko radhi kuuza karanga kuliko kwenda kuichezea timu hiyo inayosuasua kwenye ligi hiyo.
Kama hiyo haitoshi, Chuji alitishia kuchukua sheria kwa wekundu wa msimbazi ambapo kupitia kwa mwanasheria wake, alitishia kusimamisha ligi iwapo asingerejeshwa Simba, lakini Simba walibaki na msimamo wao wakutokubali kumtumia kiungo huyo sambamba kusema wameshavunja mkataba na Chuji.
Nalo Shirikisho la soka Tanzania (TFF) baada ya msigano huo, liliendelea kusisitiza kuwa Chuji ni mali ya Simba kwa kuwa aliingia nao mkataba wa kuichezea miaka miwili, pia kuwa na leseni na ndio maana akapata nafasi ya kuichezea katika michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati ‘Kombe la Kagame’.
Aidha, TFF ilisema kwamba kwa vigezo hivyo anaweza kushitaki kwao kama atajihisi kuonewa baada ya Simba kudai kuwa hawamuhitaji kwenye kikosi chao kitakachoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara kuanzia Agosti 20.
Chuji aliwahi kuichezea Simba akitokea timu ya Polisi Dodoma kabla ya baadaye kutimkiaYanga katika uhamisho uliozua mzozo mkubwa baina ya watani hao wa jadi.

1 Comments

  1. YANGA BOMBA-UHURU BRANCHNovember 10, 2011 at 4:09 PM

    YANGA NAO BWANA,WAMENIKERA SANA,HILO TEJA LA KAZI SASA JAMANI,KWANZA HI JITU LA MAJUNGU,LINAGAWA TIMU ,HALINA NIDHAMU,NAJUA NI PAPIC TU HUYO MAANA ANAVOMPENDA HUYU MTU,KI UKWELI SIJAPENDA KABISA,CHUJI HAWEZI KUWA MSAADA WOWOTE KWA YANGA,TUPO HAPA MTANIAMBIA,LILE TOTO TUNDU TU

    ReplyDelete
Previous Post Next Post