VIONGOZI wa klabu za Ligi Kuu
ya Vodacom Tanzania Bara, kesho wanatarajiwa kuwa na kikao kizito jijini Dar es
Salaam ambacho lengo lake ni kujadili
‘changa la macho’ walilopigwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Mmoja ya wajumbe wa kamati ya
Vilabu vya Ligi Kuu alisema jana kwamba wamefikia kukutana baada ya TFF
kuwahadaa kuhusu suala la kampuni ya kusimamia Ligi Kuu.
Kiongozi huyo alisema kuwa Kamati ya Ligi Kuu iliyoundwa na TFF
haikuwasilisha hoja ya Kampuni katika kikao cha Kamati ya Utendaji
kilichofanyika Februari 12, mwaka huu.
Alisema kuwa mtu ambaye anaingia kwenye Kamati ya Utendaji
ya TFF kutoka kwenye Kamati yao
ni Mwenyekiti wao pekee, Wallace Karia.
“Karia pekee ndiye Mjumbe wa
Kamati ya Utendaji ya TFF ambaye kutoka kwenye Kamati ya Ligi Kuu iliyoundwa na
TFF anaingia kwenye kikao cha Kamati ya Utendaji.
Lakini ajabu, habari ambazo
tumezipata ni kwamba hajawasilisha hoja hiyo na hakuna mtu aliyeinuka kuhoji
kuhusu suala la kampuni,” alisema kiongozi huyo.
Kiongozi huyo,pia alimlalamikia
rais wa TFF Leodegar Chillah Tenga kwa
kutotimiza ahadi zake kwa klabu ambapo alisema yeye mwenyewe atasimamia hadi
kuhakikisha suala la kampuni linaingia kwenye Kamati ya Utendaji, lakini ajabu
ameendesha kikao cha Kamati ya Utendaji bila kujadili kampuni.
“Mbaya zaidi ni kwamba, sasa
wanakwenda kwenye Mkutano Mkuu (utakaohusisha uchaguzi Mkuu pia) bila ajenda ya
kampuni,” alilalamika kiongozi huyo.
Akiizungumzia Kamati ya Ligi
Kuu, kiongozi huyo alisema kwamba ipo kama
kivuli na haihusiki na uendeshaji wa Ligi Kuu “Karia anaishi nje ya Dar es
Salaam, Ofisa waliyesema ataajiriwa, hadi leo hajaajiriwa. Kazi zote zinafanywa
na ofisi ya Sadi Kawemba kama zamani,”alisema.
Kamati ya Ligi Kuu inaundwa
na Wallace Karia (Mwenyekiti), Said Mohamed (Makamu Mwenyekiti), Damas
Ndumbaro, Yahya Ahmed, Meja Charles Mbuge, Steven Mguto, Geoffrey ‘Kaburu’
Nyange, Seif Ahmed, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Hemedi Msangi na Henry Kabera
(Wajumbe).