Shule ya Sekondari ya Makongo ya Dar es
Salaam na Lord Baden ya Bagamoyo mkoani Pwani ndizo zitakazocheza fainali ya
mashindano maalumu ya mpira wa miguu kwa wanawake kuadhimisha Siku ya Wanawake
Duniani.
Fainali hiyo itachezwa kesho (Machi 8 mwaka
huu) kwenye Uwanja wa Karume kuanzia saa 10 kamili jioni. Michuano hiyo ilianza
Februari 24 mwaka huu ikishirikisha timu nane za shule za
sekondari.
Michuano hiyo ambayo ni
maalumu kwa ajili ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani iliandaliwa na
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na Chama cha Mpira
wa Miguu cha Wanawake (TWFA).
Kundi A lilikuwa na shule za
Makongo, Goba, Twiga na Lord Baden ambapo zilichezea mechi zake za awali katika
uwanja wa Sekondari ya Makongo. Timu zilizounda kundi B na kuchezea mechi zake
uwanja wa Shule ya Sekondari Jitegemee ni Benjamin Mkapa, Jitegemee, Kibasila na
Tiravi.
Lengo lingine la mashindano
ni kuhamasisha mpira wa miguu kwa wasichana katika ngazi ya shule, kuandaa,
kubaini na kuendeleza mafanikio yanayopatikana katika timu ya wanawake ya
Taifa.
Uchaguzi wa timu shiriki
ulizingatia mchango wa shule katika kuendeleza mpira wa miguu kwa
wasichana/wanawake. Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano hayo ni Zainab Mbiro
kutoka Twiga Sekondari.