KIUNGO wa Manchester United, Paul Scholes yuko tayari
kurefusha kwa msimu mmoja, awamu ya pili ya uchezaji wake klabuni Old Trafford.
Nyota huyo mkongwe, alirejea dimbani Januari mwaka huu ikiwa ni miezi
kadhaa baada ya kustaafu soka, akifuata ombi la kocha wa United Sir Alex
Ferguson aliyekuwa ameelemewa na idadiya majeruhi zaidi kwenye idara ya kiungo.
Kurejea kwake imekuwa msaada mkubwa kwa United kwani kumeiwezesha kuwashusha mahasimu wao wa Man City katika kilele cha Ligi
Kuu ambayo ilikalia mwezi Oktoba mwaka jana.
Kwa sasa Scholes anataka kufuata nyayo za mkongwe mwenzake Ryan
Giggs (38) kiasi cha kuhitaji msimu mwingine wa kupigania heshima ya klabu hiyo
aliyopata nayo mafanikio yaliyotukuka.
Scholes amekuwa sehemu muhimu ya kikosi cha United katika
jumla ya mechi 15, kuanzia pale alipoingia akitokea benchi na kuisaidia klabu
yake kuichapa City mabao 3-2 katika mechi ya Kombe la FA iliyopigwa Januari 8.
Scholea ameanza kikosi cha kwanza mara nane kati ya mechi
hizo, akifunga mabao mawili na kuthibitisha aina ya uimara alionao. Kocha wake Ferguson
amemzungumzia akisema: "Kiwango chake kimekuwa ni cha kuvutia mno."
Scholes alistaafu soka mwishoni mwa msimu uliopita, lakini
ghafla akalalamika kutojisikia vema kuukosa mchezo aupendao, wakati huo akibeba
jukumu la kukinoa kikosi cha nyota wa akiba wa United kwenye uwanja wa Carrington.