Kikao cha Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF, iliyoketi
kusikikiza mashitaka dhidi ya Alhaj Ismail Aden Rage na Louis Sendeu
kilifanyika leo tarehe 24 Machi, 2012 kilisikiliza tuhuma zilizowasilishwa na
TFF. Mashitaka hayo yalihusiana na matamko yaliyotolewa na watuhumiwa hao kabla
ya mchezo wa Ngao ya Hisani kati ya Simba na Yanga, uliochezwa tarehe 17
Agosti, 2011.
Katika mashitaka hayo, watuhumiwa hao walituhumiwa kukiuka
Kanuni ya 30 (1) (f) na Kanuni ya 53 (1) (2) cha Kanuni za Adhabu za FIFA.
Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili na kutafakari
maelezo hayo, pamoja na kuchambua sheria na kanuni mbalimbali, Kamati imeamua
yafuatayo:
Hasara kwa Mdhamini
Kuhusiana na suala hasara, Kamati inaona kwamba suala hili
halikuwa na uzito wowote wala hakukuwa
na hoja ya msingi, wala ushahidi wa kuthibitisha kwamba tishio au matamko hayo
yalikuwa na uhusiano na hasara inayodaiwa kwamba mdhamini huyo aliipata. Hakuna
malalamiko yoyote yaliyotolewa kuhusiana na kinachodaiwa kuwa ni hasara
inayotokana na matamko ya viongozi hawa. Kamati imeitupilia mbali hoja hii.
Tuhuma za matamko ya watuhumiwa
Kamati imebaini kwamba matamko hayo yalikuwa ni uvunjaji wa
kanuni na yalilenga kuchochea hisia mbaya na kuleta vurugu. Kamati ina maoni ya
kwamba viongozi wa vilabu hivi walistahili kufuata taratibu za kawaida katika
kudai haki zao, badala ya kutoa matamko ambayo yangeweza kuchochea hisia mbaya. Kitendo hicho si cha kiungwana
na kinaendana kinyume na taratibu za uongozi wa mpira.
Wao kama viongozi, walistahili kutumia utashi na kupima
athari za matamko yao, ili kuepuka uwezekano wa kuleta msuguano usio wa lazima
na kuungiza mchezo wa mpira katika kashfa au kukosa heshima. Matamko haya
yanaweza kuwa ni kichocheo kwa viongozi wengine wenye tabia ya namna hiyo kutumia
mwanya huu kufanya vitendo hivyo.
Kwa msingi huo, Kamati inawaona wote wawili kuwa wana hatia
na matamko hayo yanayohusiana na mchezo huo. Kwa kuzingatia hilo, Kamati inatoa
onyo kali dhidi ya watuhumiwa hao wawili na inaonya kwamba adhabu kali zaidi
zitachukuliwa kama watuhumiwa watalirudia kosa kama hili au linalofanana na
hilo.
Kamati imebaini pia kwamba Mheshimiwa Aden Rage amehusika
pia na kutoa maneno ya uchochezi dhidi ya Bwana Saad Kawemba wa TFF, akidaiwa
kwamba alikuwa anazuia usajili wa mchezaji Gervais Kago na kwamba Bwana Kawemba
alifanya hivyo kwa vile ana mapenzi na klabu ya
pinzani ya Yanga.
Pamoja na kwamba hakukuwa na athari za moja kwa moja dhidi
ya Bwana Kawemba, ukweli ni kwamba kitendo hicho kilikuwa ni kosa ambalo
halistahili kufanywa na kiongozi mwenye uzoefu mkubwa wa uongozi kama
Mheshimiwa Rage, na kilikuwa kina dalili za kuchochea chuki zisizo na msingi
dhidi ya Bwana Kawemba. Kitendo hicho kilikuwa kinakiuka kifungu cha 53 (1) (2)
cha Kanuni za Adhabu za FIFA.
Kamati inatoa onyo kali dhidi ya Mheshimiwa Aden Rage kwa
kupatikana na hatia yake hiyo.
Imetolewa na Kamati ya Nidhamu na usuluhishi leo tarehe 24
Machi, 2012.
..................................................
Kamishna Alfred Tibaigana
Mwenyekiti wa Kamati