WAWAKILISHI wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga, leo
watakuwa na kibarua kigumu watakaposhuka Uwanja wa Jeshi jijini Cairo, Misri,
kukwaana na wenyeji Zamalek ikiwa ni mechi ya marudiano raundi ya kwanza.
Yanga ambayo iliwasili Cairo tangu juzi na kufikia Hoteli ya Holiday
Inn, ilikumbana na baridi kali iliyofikia nyuzi joto 16 na kuonekana kuwachosha
wachezaji na viongozi, ambao hawakutarajia kukutana na hali kama hiyo.
Pamoja na hali hiyo, wawakilishi hao kupitia kwa Mwenyekiti wao, Lloyd
Nchunga, wameapa kucheza kwa nguvu zote, kuhakikisha wanashinda mchezo huo na
hatimaye kusonga mbele.
“Tunashukuru tumefika salama, lakini kwa bahati mbaya tumekutana na
baridi kali sana…hata hivyo hali hii isiwatie hofu Wanayanga, kuwa timu yetu
itashindwa kuhimili mikikimikiki ya huku,” alisema Nchunga katika mahojiano
yake na mtandao mmoja wa nchini Misri.
Katika mchezo wa leo, Yanga huenda ikawakilishwa na Shaban Kado, Nahodha
Shadrack Nsajigwa, Stefano Mwasyika,
Athumani Iddi ‘Chuji’, Nadir Haroub Ali ‘Cannavaro’, Juma Seif ‘Kijiko’,
Haruna Niyonzima, Omega Seme, Hamisi Kiiza, Kenneth Asamoah na Davies Mwape.
Pia nyota wengine wa Yanga walio huko ni pamoja na Chacha Marwa, Nurdin
Bakari, Shamte Ally, Jerry Tegete, Pius Kisambale, Oscar Joshua na Job Ibrahim,
ambao wote wako fiti.
Yanga inayonolewa na Mserbia, Kostadin Papic, inatakiwa kucheza kwa
umakini mkubwa kutokana na wapinzani wao kuwa na nyota wengi wenye uzoefu na
uwezo mkubwa.
Yanga inahitaji ushindi au sare ya mabao 2-2 kuitoa Zamalek kwenye
michuano hiyo ambapo katika mchezo wa awali uliopigwa jijini Dar es Salaam timu
hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
Yanga haijawahi kuifunga timu yoyote ya Misri tangu ianze kukutana nazo
mwaka 1982.
Mafanikio makubwa kwa Yanga katika michuano ya Afrika ni kucheza hatua
ya makundi ya Ligi ya Mabingwa 1998 na wakati michuano hiyo ikiitwa Klabu
Bingwa Afrika, walicheza robo fainali mara mbili 1969 na 1970 na pia Robo
Fainali ya Kombe la Washindi mwaka 1996.