WAGANDA KUCHEZESHA NGORONGORO VS
SUDAN
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Afrika (CAF) limewateua waamuzi kutoka Uganda kuchezesha mechi ya michuano ya
Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 kati ya Tanzania (Ngorongoro
Heroes) na Sudan itakayofanyika Aprili 21 mwaka huu.
Mwamuzi atakayechezesha mechi
hiyo itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni ni
Brian Miiro. Waamuzi wasaidizi ni Mark Ssonko na Lee Patabali wakati mwamuzi wa
mezani ni Denis Batte.
Ejigu Ashenafi wa Ethiopia
ndiye ameteuliwa kuwa Kamishna wa mechi hiyo namba 15. Kamishna na waamuzi hao
watawasili nchini Aprili 19 mwaka huu kwa ndege za Ethiopian Airlines na Air
Uganda.
KINYANG’ANYIRO VPL KUENDELEA
APRILI 18
Kinyang’anyiro cha Ligi Kuu
ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara kinaendelea tena kesho (Aprili
18 mwaka huu) kwa mechi tano zitakazochezwa kwenye miji ya Bukoba, Mwanza, Dar
es Salaam, Mlandizi na Dodoma.
Mabingwa watetezi Yanga watakuwa wageni wa
Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba wakati Toto Africans
itaikaribisha African Lyon kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Vinara wa ligi hiyo Simba
wataoneshana kazi na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, Ruvu
Shooting na Moro United zitaumana kwenye Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi. Nayo
Polisi Dodoma itakuwa mwenyeji wa Coastal Union mjini Dodoma.
TENDA YA TIKETI KUFUNGULIWA
APRILI 18
Sekretarieti ya Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kesho (Aprili 18 mwaka huu) itafungua maombi ya
tenda zilizowasilishwa na kampuni mbalimbali kwa ajili ya kutengeneza tiketi za
elektroniki.
Maombi hayo yatafunguliwa saa
9 alasiri kwenye ofisi za TFF ambapo kampuni zote zilizowasilisha tenda
zinatakiwa kuwepo wakati wa ufunguzi huo.
Machi 9 mwaka huu TFF
ilitangaza tenda kwa ajili ya kutengeneza tiketi za elektroniki kwa ajili ya
mechi za Ligi Kuu ya Vodacom na mechi nyingine azozisimamia.