Meneja wa bia ya Kilimanjaro George Kavishe akifafanua jambo kuhusiana na ziara hiyo, kushoto ni mshindi wa Tuzo tatu, Diamond.
WASANII walioshinda tuzo za muziki za Kili
mwaka 2012 pamoja na wale waliokuwa wakiwania tuzo hizo wanatarajiwa kufanya
ziara maalum katika mikoa sita ili kutoa shukrani kwa mashabiki sambamba na
kuwapa burudani.
Meneja wa bia ya Kilimanjaro inayozalishwa na kampuni ya bia Tanzania (TBL)
George Kavishe alisema kwamba lengo la ziara hiyo pia ni kuwapa fursa mashabiki
wa sehemu husika kuwashuhudia wasanii hao kwa njia ya burudani.
Alisema katika mikoa ambayo wasanii
hao watapita kutaendeshwa zoezi la kuwapata wasanii chipukizi ambapo kila mkoa
utatoa msanii mmoja ambaye baadaye atakuja jijini Dar es Salaam kurekodi na
mmoja ya wasanii maarufu.
Alisema mchakato wa kuwapata wasanii
hao chipukizi utaendeshwa katika tarehe maalum zilizopangwa katika kila mkoa
husika huku majaji wakitarajiwa kuwa wasanii wa muziki wa bongo fleva wakiwemo
Profesa J, Juma Nature na Queen Darleen.
Kavishe aliongeza kuwa ziara hiyo
inatarajiwa kuanza Aprili 28 mkoani Dodoma katika Uwanja wa Jamhuri, wakati Mei
7 itakuwa katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Kilimanjaro itakuwa Mei 12
kwenye Uwanja wa Ushirika na Mbeya itakuwa Mei 19 katika Uwanja wa
Sokoine.
Aidha wakazi wa Mtwara watapata
fursa hiyo Mei 26 katika uwanja wa Mtwara kabla ya
ziara hiyo kuhitimishwa Juni 2 kwenye viwanja vya Leaders jijini Dar
salaam.
Baadhi ya wasanii watakaoshiriki
katia ziara hizo ni pamoja na Diamond, Isha Mashauzi, Ali Kiba, At, bendi ya
Twanga Pepeta, Ben Pol, Kalidjo Kitokololo, Ommy Dimples, Khadija Kopa, Suma
Lee, Jaguar, Barnaba, Warriours from the East, Queen Darlin na wengineo.
Kwa upande wake msanii aliyefanikiwa kutwaa
tuzo tatu mwaka huu Nassib Abdul ‘Diamond’ akizungumza kwa niaba ya wasanii
wenzake pamoja na kushukuru kwa mashabuiki kumuwezesha kutwaa tuzo hizo,
aliwaomba mashabiki kujitokeza kwa wingi katika maeneo ambayo watapita kufanya
maonyesho.