Makala Ratiba Ligi Kuu inatoa mwanya upangaji matokeo Imeandikwa na Jemedari Said; Tarehe: 27th April 2012 @ 14:59 Imesomwa na watu: 120; Jumla ya maoni: 0 |
Ni katika hali ya kushangaza sana hili linatokea huku kukiwa na timu ambazo zinagombea ubingwa kwa kiwango sawa na zingine zikiwa zinapigana ili zisishuke daraja. Timu za Azam na Simba za Dar es Salaam ndizo pekee zenye nafasi ya kuwa mabingwa wapya baada ya bingwa mtetezi Yanga kuvuliwa ubingwa. Hali ikiwa hivyo, Azam imebakiza mechi mbili dhidi ya Kagera Sugar na Toto Africans ambazo zote zitapigwa kwenye uwanja wa Azam pale Chamazi. Kama Azam itafanikiwa kushinda mechi zote mbili itakuwa imefanikiwa kufikisha alama 59 ambazo tayari Simba wanazo, lakini wakiwa na mchezo mmoja mgumu mkononi dhidi ya watani zao, Yanga. Kama Simba watafungwa dhidi ya Yanga na Azam kushinda zote, basi bingwa atapatikana kwa uwiano wa magoli ya kufunga na kufungwa. Kwa kulielewa hili na katika ligi hii ya kuuza na kununua, hali hii inawapa nafasi kubwa klabu ambayo inabakiwa na mechi nyingi kupata nafasi ya kufaidika kwa kupanga matokeo na kuzifunga timu nyingine idadi kubwa ya mabao. Kwa mfano, Azam imebakiza mechi ambazo kimtazamo ni dhaifu, ingawa kiuhalisia inawezekana kuwa si dhaifu kihivyo, lakini wako na faida ya kujua au hata kuhisia idadi gani ya mabao inaweza kuwafanya kuwa mabingwa. Kwenye ligi hii ambayo kila uchao kunakuwa na shutuma za aidha marefa kupanga matokeo kwa kuzipendelea baadhi ya timu, hali ambayo inahusishwa na utoaji wa pesa, hakukutakiwa hali kama hii itokee katika hatua hii ya mwishoni mwa ligi ili kuepusha mazingira ya kupanga matokeo iwe ni kwa timu zinazogombea ubingwa au zile ambazo zina hali mbaya kwa misingi ya kushuka daraja. Tayari hapo tulipo kuna tuhuma dhidi ya baadhi ya klabu zinatumia sana pesa kwa kuwahonga marefa au hata wachezaji wa timu pinzani ili kupata urahisi wa kushinda mechi zao. Nakubaliana na Shirikisho la Soka nchini (TFF) kwamba inakuwa vigumu kwao kuzifanyia kazi tuhuma hizi kwani zinakuwa hazina uthibitisho wa kutosha kuweza kuwatia hatiani watuhumiwa, lakini sidhani kama walitakiwa wazipuuze kabisa tuhuma hizi. Kwa hali inavyoonekana ni kama vile tuhuma hizi kwao wao hazina maana wala umuhimu wowote ingawa waamuzi kweli wanaharibu tena katika mazingira ya kutia shaka na wao kupitia kamati zao sio tu wanawafungia, lakini pia wanafikia hatua hata ya kuwafuta kabisa. Sikutegemea kwa kulijua hili bado wangeendelea kutoa nafasi kwa mazingira ya rushwa kuendelea kuwepo katika ratiba zao za ligi. Ratiba kama inavyoonesha hapo ni kwamba mazingira ya rushwa hayakwepeki na kwa kuwa imekuwa ngumu kwao kuwabaini watuhumiwa, itakuwa bado ngumu kwao kuzuia hii mianya ambayo ipo wazi kabisa. Kwa mawazo yangu nilidhani kwamba mechi zote zinazohusu timu zilizo kwenye mazingira ya kushuka daraja na zile zenye nafasi ya kuwa bingwa zilistahiki kuchezwa kwa siku moja na wakati unaofanana. Najua hii inaweza isiwe tiba, lakini walau ingesaidia kupunguza mianya ambayo sasa inaonekana wazi. Katika hali ilivyo sasa sio tu kwamba timu yenye mechi nyingi mkononi inakuwa na mazingira ya kushinda, lakini pia inakuwa kwa namna nyingine kwenye hali ngumu ya kushinda mechi zake kwani ni wazi kwamba timu ambayo inapigania ubingwa na imepata alama zake nzuri kibindoni, inaweza kutumia muda huu ‘kuzicheza’ mechi za hasimu wake ili asifikie kule aliko kitu ambacho kinageuza mechi za timu pinzani kuwa ngumu kuliko maelezo. Kila mara kumekuwa kukitokea hii hali ya timu fulani kuunga urafiki wa kinafiki na timu ambayo inacheza na mshindani wake kwenye kutwaa ubingwa, kwa kujifanya inaisaidia na kuipa motisha ili ishinde kwa kuwapa ahadi ya pesa kama itafanikiwa aidha kushinda au hata kupata sare. Hili linakuwa tatizo katika mpira wetu, na kwakuwa halifanyiki kwa kificho nilidhani TFF walitakiwa kuliangalia kwa jicho la ziada ili kukwepa kutoa mianya ya wazi. Hali kama ilivyo sasa ni dhahiri kwa mpira wa Tanzania kwamba, mechi ya Azam na Kagera Sugar itakuwa ngumu kwa Azam kwani watu wa fitina lazima ‘wataicheza’ ili kuzuia Azam kushinda kirahisi na kwa magoli mengi ambayo yataathiri nafasi yao ya kutwaa ubingwa. Hili liko wazi na wala watendaji wa TFF wasijifanye ‘hamnazo’ na kujitia ugeni usio wao kwamba eti wao hawajui kwamba hawa miamba wa nchi hii wanaongoza kwa kucheza nje na ndani na hata ‘kuzicheza’ mechi za wenzao. Hakuna mgeni katika mpira wa Tanzania pale TFF kiasi cha kwamba anaweza asijue kwamba kuna hii hali, isipokuwa ni kwamba hata hapo kwenye shirikisho lenyewe tayari watu wamegawanyika na timu zao, kuna kipindi wanafanya kwa maslahi ya hizi timu ili kuzifurahisha nafsi zao. Kuna baadhi ya timu ziko kwenye ligi hii ya Vodacom kwa miaka zaidi ya kumi wao kazi yao ni kutafuta alama ambazo zitawabakisha kwenye ligi tu, baada ya hapo wanakuwa kwenye mazingira ya kutengeza pesa tu. Hizi zinajulikana na zimekuwa zikishutumiwa waziwazi na si kweli kwamba watendaji wa TFF wao hawajawahi kuzipata tuhuma hizi! Kupunguza hali hii ni kutotoa mianya ya wazi kama ilivyo kwa ratiba ya sasa. jkazumari@gmail.com 0713 528 790 |