CD MAZISHI YA KANUMBA MARUFUKU, STAR TIMES YATOA UBANI


SHIRIKISHO la filamu Tanzania (TAFF) litamchukulia hatua mtu yoyote atakayebainika kuuza CD za shughuli ya mazishi ya aliyekuwa msanii wa filamu nchini marehemu Steven Kanumba bila kupata ridhaa toka kwa familia yake.
Rais wa Taff Simon Mwakifambwa alisema hayo jana mbele ya familia nyumbani kwa marehemu Sinza Vatican.
Alisema marehemu alikuiwa akitegemewa na familia kupitia kazi zake za filamu hivyo kama hakutakuwa na usimamizi mzuri wa kazi zake familia itayumba.
Aliongeza kuwa kama Cd hizo zitasimamiwa vema zitaingiza fedha ambazo zitasaidia kuendesha familia hiyo hivyo ametoa tahadhari kwa wanaotaka kufanya ujanja huo na kuongeza kuwa wanazao taarifa tayari wameanza kufanya uchunguzi.

Katika hatua nyingine kampuni ya ving’amuzi ya StarTimes imetoa sh milioni 1.6 kama ubani kwa ajili ya kifo cha  Kanumba, aliyefariki usiku wa kuamkia Aprili 7 jijini Dar es Salaam.
Akikabidhi msaada huo, Meneja Masoko wa Kampuni hiyo, Zuhura Hanifu, alisema wameguswa na msiba wa msanii huyo.
“Tumeguswa kwa kiasi kikubwa na msiba wa msanii huyo kutokana na kufanya kazi katika kampuni yetu kwa muda mrefu,” alisema.
Zuhura alisema ni wazi Kanumba ameacha pengo kubwa ambalo halitaweza kuzibika kwenye kampuni hiyo.
Aliongeza kuwa Kanumba ameisaidia kampuni yao, kwa kiasi kikubwa, kuitangaza kupitia promosheni mbalimbali ambapo pia alikuwa ni balozi wa StarTimes hadi mauti yake yanamkuta.
Kanumba alizikwa katika makaburi ya Kinondoni, Aprili 10, mwaka huu; mazishi yaliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na maelfu ya wananchi wakiwamo wapenzi na mashabiki wa filamu.

Post a Comment

Previous Post Next Post