Na Ahmed Khatib ,Tanga
TIMU ya Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’ ya jijini hapa,
imekabidhiwa basi lenye thamani ya sh milioni 45 na kampuni ya saruji ya Tanga,
jana.
Akikabidhi basi hilo kwa
viongozi wa Coastal, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanga Cement, Erik Westerberg, alisema, basi hilo wamelitoa kutokana
na juhudi zilioneshwa na timu hiyo katika Ligi Kuu ya soka Tnzania Bara
inayoelekea ukingoni.
“Msaada huu wa leo, nina imani kuwa utaongeza ari na nguvu
ya kujituma zaidi katika michezo iliyobaki, kwani mafaniko yenu ndio mafaniko
ya Tanga Cement na tunaahidi kufanya mazuri zaidi, ikiwa na nyie mtaonyesha
moyo wa kizalendo kwa timu yenu kufanya vizuri zaidi,” alisema Westerberg.
Hata hivyo, Westerberg, alitoa rai kwa viongozi wa klabu
hiyo watambue kuwa, basi hilo ni kwa matumizi ya
timu tu na sio mengine binafsi, huku akiwataka kulitunza kwa maendeleo ya timu yao .
Naye Mwenyekiti wa Coastal Union, Hemed Aurora, alisema,
msaada kampuni hiyo waliyoutoa, ni wa kwanza katika kipindi hiki na hiyo ni
kutokana na kikosi hicho kufanya vizuri katika ligi.
Kwa upande wake, Nahodha wa timu hiyo, Said Sued,
aliwahakikishia mashabiki wao kuwa, watahakikisha wanabaki nafasi ya nne
mwishoni mwa ligi kuu, huku akisisitiza umoja na mshikamo kwa viongozi na
wachezaji wenzie, kuwa ndio siri kubwa ya mafanikio.
Timu hiyo, kwa sasa inaendelea na mazoezi kwenye uwanja wa
Mkwakwani kwa maandalizi ya mchezo wake unaofuata dhidi ya Villa Squad
utakaochezwa jijini Dar es Salaam
wiki hii.