HATIMAYE
mdau mkubwa wa klabu ya soka ya Simba Azim Dewji leo amekabidhi kitita cha
shilingi milioni 15 kwa wachezaji wa klabu hiyo kama zawadi ya kutinga 16 bora
ya kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF).
Dewji
amekabidhi fedha hizo baada ya mtandao huu jana kuripoti taarifa za mfadhili
huyo wa zamani wa Simba kupiga chenga kutimiza ahadi hiyo aliyoitoa wiki
iliyopita baada ya Simba kutinga hatua hiyo kwa kuiondoa Es Setif ya Algeria.
Habari
kutoka katika kambi ya klabu ya Simba iliyopo Bamba Beach Kigamboni jijini Dar
es Salaam zinaeleza kuwa Dewji alitinga kambini hapo asubuhi ya leo na
kukabidhi fedha hizo kwa viongozi wa benchi la ufundi la Simba.
Taarifa
zinaeleza kuwa Dewji aliwaeleza wachezaji hao kuwa alishindwa kutoa fedha hizo
kwa wakati aliopanga kutokana na kusubiri kuanza kwa kambi ambapo aliamini
wachezaji wangekuwepo wote.
“Tunashukuru
bwana Dewji hatimaye amepeleka zile fedha alizokuwa akizitangaza kwenye vyombo
vya habari kuwa atawapa wachezaji kutokana na kusonga mbele kwenye kombe la
CAF,”Aliongeza kiongozi huyo.
Katika
hatua nyingine, kikosi cha wachezaji wa timu hicho kilichopo kambini
kinaendelea na maandalizi yake ya michezo yake ya ligi kuu soka Tanzania Bara
na ule wa Shirikisho dhidi ya Al Ahly Shandy ya Sudan Aprili 22 kwenye uwanja
wa Taifa, jijini Dar es Salaa.
Simba
inayoongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 50 keshokutwa itashuka katika dimba la
Taifa jijini Dar es Saalam kukwaana na maafande wa Ruvu Shooting.