MBUNGE
wa Kinondoni, Iddi Azan, (CCM), amemuumbua Naibu Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, kutokana na kutoa taarifa za
kupotosha bungeni kuhusu timu zilizoshinda katika Kombe la Chalenji na Klabu
Bingwa Afrika Mashariki na Kati.
Akitoa
taarifa bungeni jana, mbunge huyo alisema, si kweli kwamba timu ya taifa,
ilitwaa kombe hilo
mara tano na timu za Simba na Yanga, zilishinda Kombe la Klabu Bingwa Afrika
Mashariki na Kati mara moja kwa kila timu.
Azan alisema usahihi ni kwamba, Simba ilishinda kombe
hilo mara sita na Yanga mara tano, huku timu ya taifa ilishinda mara tatu Kombe
la Chalenji, mwaka 1974, 1994 na mwaka 2011.
“Nimesikitishwa na majibu yaliyotolewa na serikali
kuhusu matokeo ya michuano hiyo. Naomba kutoa taarifa Naibu Spika,” alisema
Azan.
Katika swali la msingi la Mbunge wa Ziwani, Ahmed
Ngwali, aliyetaka kujua ni mafanikio gani ya msingi na ya kujivunia
yaliyopatikana kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), mpaka sasa.
Akijibu swali hilo, naibu waziri huyo alisema kwa
jumla shirikisho hilo limefanikiwa kukuza na kuendeleza mpira wa miguu kila
kona ya nchi na kuweka muundo wa utawala katika kila ngazi, kuandaa wataalamu
wa fani za ufundishaji, uamuzi, utawala na tiba kwa wanamichezo zaidi ya 10,000
na kuongeza kuwa, wataalamu hao wamepata mafunzo hayo tangu nchi ilipopata
Uhuru.
“Shirikisho pia limefanikiwa kuandaa na kuendesha
programu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mashindano ya timu za vijana, wanawake
na watoto kama sehemu ya kuweka msingi bora wa maendeleo ya mchezo wa soka,”
alisema.
Pia alisema timu ya taifa ilifanikiwa kucheza mara
moja fainali za Kombe la Afrika na mara moja kwa timu za taifa za wachezaji wa
ligi za ndani, (CHAN), pamoja na kujenga na kuimarisha uhusiano mwema kati ya
shirikisho na serikali.