PAPIC OUT, TIMBE INN AGAIN YANGA


Papic
UONGOZI wa mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania Bara, Yanga uko mbioni kumrejesha kukinoa kikosi hicho aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mganda Sam Timbe.
Timbe ambaye aliiwezesha Yanga kutwaa ubingwa wa ligi kuu msimu wa 2010/2011 na kombe la Kagame, mkataba wake ulivunjwa msimu uliopita kwa madai ya kushindwa kuiletea mafanikio timu hiyo na nafasi yake kujazwa na Mserbia Kostadin Papic.
Habari za uhakika kutoka ndani ya klabu hiyo yenye maskani yake mitaa ya Jangwani na Twiga zinaeleza kuwa Timbe atarejea kukinoa kikosi hicho wakati wowote kuanzia sasa akirithi mikoba ya Papic.
Imeelezwa kuwa mkataba wa Papic umebakiza siku chache kumalizika na uongozi hauna mpango wa kumuongeza mkataba mkataba mpya,kutokana kutomuhitaji tena.
Mmoja ya viongozi wa Yanga ambaye hakupenda kutajwa jina lake aliliambia gazeti hili kwamba hawana mpango tena na Papic kutokana na kutokuwa na jipya ndani ya klabu hiyo hivyo wanaendelea na mikakati ya kumrejesha Timbe.
“Mimi nashangaa huyu kocha anazungumza na vyombo vya habari kuwa hajalipwa miezi mitatu, huo ni uzushi ambao hauna maana yoyote...ninachoona ni kutaka kuudanganya umma ili adanganye kuwa kaondoka kwa kutolipwa wakati mkataba wake ulishakwisha,”Aliongeza.
Baadhi ya vyombo vya habari leo viliripoti kocha hutyo kutoambatana na timu Kanda ya Ziwa kutokana na kuugua Tumbo na mafua huku pia ikidaiwa kocha huyo hajalipwa mshahara wake kwa miezi mitatu hali inayomuweka katika mazingira magumu ya ufundishaji wake.
Hata hivyo ofisa habari wa Yanga Louis Sendeu alisema jana kuwa taarifa za Papic kudai mshahara hazina ukweli wowote na kukiri kuwa kocha huyo ni mgonjwa ndio maana hajaambatana na timu katika safari hiyo , lakini kama hali yake itatengemaa huenda akaungana na timu hiyo leo.
Alisema kikosi cha timu hiyo kinanatarajiwa kuondoka Kahama leo kwenda Mwanza tayari kwa mechi yao ya Ligi Kuu soka Tanzania Bara ambapo jumapili kitashuka kwenye dimba la CCM Kirumba, jijini humo kukwaana na wenyeji Toto African.

Post a Comment

Previous Post Next Post