Azim |
UONGOZI wa klabu ya Simba
umeshangazwa na taarifa zinazotolewa na aliyewahi kuwa mfadhili wa timu hiyo, Azim Dewji
kuhusiana na kutoa fedha kwa wachezaji wa timu hiyo, sambamba na kuileta timu
ya Tp Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) .
Hatua hiyo inafuatia hivi
karibuni Dewji kukaririwa na vyombo vya habari kutoa shilingi milioni 15 kwa
ajili ya kuipongeza Simba kutokana na kutinga hatua ya pili ya kombe la
Shirikisho Afrika (CAF) baada ya kuitoa Es Setif ya Algeria wiki, pia kuileta
TP Mazembe kwa ajili ya kucheza mechi ya kirafiki na Simba.
Mmoja ya viongozi wa Simba (jina
tunalo) amesema leo kuwa Dewji amekuwa akifanya mambo kinyemela hali ambayo
inasababisha kuwepo kwa mvurugano usio na maana ndani ya klabu hiyo.
Akifafanua zaidi, kiongozi huyo
alisema kuwa hata zile fedha za awali (sh.mil.15) ambazo ilidaiwa kuwa amewapa
wachezaji hazikuwa na ukweli wowote kwani fedha hizo zilitolewa na uongozi.
“Nakumbuka Azim alikuja kuongea
na wachezaji baada ya mchezo wetu na Es Setif hapa nyumbani na kuahidi kutoa
mil.15 lakini hakuzitoa na matokeo yake wachezaji walipomfata alidai kuwa hana
fedha mpaka mwisho wa mwezi.
“Hata hivyo Dewji hakutoa hiyo
hela na tuliposhinda Algeria alidai atawapa wachezaji Mil.15 pindi
watakaporejea, lakini timu imerejea tangu jumatatu na mpaka hii leo (jana)
hakuna kitu kama hicho hata taarifa za viongozi kukabidhiwa hizo hela ni uongo
mtupu,”Aliongeza.
Aidha kiongozi huyo aliongeza
kuwa hata taarifa za Dewji kuileta TP Mazembe kwa ajili ya kuja kuipa makali
Simba kabla ya mechi yake ya kombe la Shirikisho dhidi ya Al Ahly Shandy ya
Sudan hawana taarifa nazo zaidi ya kuzisoma tu kwenye magazeti.