Kamati ya
Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana jana (Aprili
17 mwaka huu) imetupa rufani ya Yanga iliyowasilishwa mbele yake kupinga uamuzi
wa kupokwa pointi tatu kwa kumchezesha mchezaji asiyestahili.
Aprili 2
mwaka huu Kamati ya Ligi ya TFF iliipa Coastal Union ushindi wa pointi tatu na
mabao matatu baada ya Yanga kumchezesha beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kwenye
mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya timu hizo iliyofanyika Machi 31
mwaka huu wakati akiwa na adhabu ya kukosa mechi tatu.
Yanga
katika rufani hiyo iliwasilisha sababu nane za kupinga kupokwa pointi
hizo, kubwa zikiwa Cannavaro hakustahili
kutumikia adhabu ya kukosa mechi tatu, si aliyempiga refa Israel Nkongo, ripoti
za refa na kamishna wa mechi yao dhidi ya Azam zilionesha dalili ya njama
(conspiracy) kwani zilifanana.
Pia
Cannavaro alikuwa miongoni mwa wachezaji ambao adhabu zao zilisimamishwa na
Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu, Kamishna mstaafu wa Polisi, Alfred Tibaigana.
Katika
uamuzi wake, Kamati imesema adhabu ya Cannavaro ya kukosa mechi tatu kwa mujibu
wa Kanuni ya 25(c) ya Ligi Kuu ya Vodacom ilitolewa na refa na si Kamati ya
Ligi kama ambavyo inalalamikiwa na Yanga, na kanuni hiyo haikatiwi rufani.
Pia barua
ambayo TFF iliiandikia Yanga kuhusu adhabu ya mchezaji huyo ilikuwa wazi kwani
ilikariri kanuni ya 25(c), hivyo kitendo cha klabu hiyo kumtumia mchezaji huyo
ulikuwa ni uzembe wa kutoheshimu kanuni. Kama Yanga haikufahamu vizuri kanuni
hiyo ilikuwa na fursa ya kuiandikia TFF kwa mujibu wa Kanuni ya 25(f) ili
kupata ufafanuzi kabla ya kuamua kumtumia mchezaji huyo.
Vilevile
adhabu zilizokuwa zimesimamishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu ni zile
ambazo zilikuwa zimetolewa na Kamati ya Ligi, na si zile zilizotolewa uwanjani
na refa.
Kuhusu
madai ya conspiracy kwa ripoti za kamishna wa mchezo huo na refa, Kamati
imebaini kuwa hazifanani, na suala lililokuwa likibishaniwa (contentious issue)
lilikuwa ni kunyang’anywa pointi tatu.
Pia Kamati
ilikariri Ibara ya 50 ya Kanuni za Nidhamu za Shirikisho la Kimataifa la Mpira
wa Miguu (FIFA) kuwa mchezaji anayembughudhi refa kwa njia yoyote ile
anastahili kufungiwa kwa angalau mechi sita.
Boniface
Wambura
Ofisa
Habari
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
haya bhana! hongera kwa hili tibaigana
ReplyDelete