BAADA ya kupoteza harakati za kutetea ubingwa wa Ligi Kuu soka Tanzania
Bara, Yanga imejinasibu kushinda michezo yake iliyosalia kwenye ligi hiyo ili
kulinda heshima.
Yanga ambayo kesho itashuka katika uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam
kuwakabili maafande wa Polisi Dodoma, iliweka rehani ubingwa wake huo baada ya
vipigo viwili mfululizo ambapo walianza kutandikwa bao 1-0 na Toto African,
kabla ya kufungwa tena bao 1-0 na Kagera Sugar ya Kagera.
Ofisa habari wa Yanga Loius
Sendeu ameiambia mamapipiro blog kuwa pamoja na kufanya kwao vibaya kwenye michezo iliyopita
bado wamerekebisha makosa ili kushinda mechi zilizosalia.
“Kufanya kwetu vibaya katika mechi mbili zilizopita na hatimaye kupoteza
matumaini ya kutetetea ubingwa si tatizo, kikubwa ni kwamba tumejipanga
kushinda ili kulinda heshima,”alisema Sendeu.
Sendeu aliongeza kwamba kikosi cha timu hiyo kipo katika hali nzuri ambapo
jana asubuhi kilifanya mazoezi katika uwanja wa Kaunda jijini Dar es Salaam.
Yanga inashika nafasi ya tatu kwenye ligi hiyo ikiwa na pointi 43 nyuma
ya Azam Fc yenye pointi 50 huku Simba inayoongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 56.