CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo
Tanzania (TASWA) Jumapili Mei 20, 2012 saa nne asubuhi kitatangaza mdhamini wa
Tuzo za Mwanamichezo Bora wa Tanzania kwa mwaka 2011.
Mdhamini huyo
atatangazwa kwenye mkutano ambao ataufanya Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto
pamoja na mdhamini wa tuzo hizo, ambapo mkutano huo utafanyika kwenye mgahawa
mpya uitwao City Sports & Lounge uliopo jirani na mnara wa askari makutano
ya barabara ya Samora na Azikiwe, Posta Dar es Salaam.
TASWA inachukua
fursa hii kuwaalika waandishi wote wa habari za michezo kuhudhuria kwenye
mkutano huo ili tuweze kuanza pamoja katika mbio hizi za kuelekea kwenye Tuzo ya
Mwanamichezo Bora wa Mwaka 2011.
Tayari Kamati ya Tuzo ishateuliwa na
imetangazwa, hivyo baada ya mkutano huo taratibu nyingine zitatangazwa kwa kadri
zitakavyokuwa zimekamilishwa na Kamati Maalum ya Tuzo ya Mwanamichezo Bora wa
Tanzania .
Kwa miaka mitano
iliyopita walioshinda Tuzo ya Mwanamichezo Bora wa TASWA walikuwa ni Samson
Ramadhani (2006), Martin Sulle (2007), Mary Naali (2008), ambao wote ni
wanariadha, wakati 2009 na 2010 alikuwa mcheza netiboli Mwanaidi
Hassan.