NGORONGORO HEROES KWENDA SUDAN KESHO


Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) inatarajia kuondoka kesho (Mei 2 mwaka huu) kwenda Sudan kwa ajili ya mechi dhidi ya Sudan itakayochezwa Mei 5 mwaka huu. 
Msafara wa Ngorongoro Heroes utakaokuwa na watu 28 ukiongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Athuman Kambi utaondoka saa 8.45 mchana kwa ndege ya Kenya Airways. 
Ngorongoro Heroes itaagwa rasmi kwa kukabidhiwa Bendera ya Taifa kesho (Mei 2 mwaka huu) saa 5 kamili asubuhi kwenye ofisi za TFF zilizoko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume. 
Wengine katika msafara huo ni wachezaji na benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Kim Poulsen. Mechi hiyo ya marudiano namba 16 itachezwa kwenye Uwanja wa Khartoum kuanzia saa 2 kamili usiku kwa saa za Sudan. 
Iwapo Ngorongoro Heroes ambayo ilishinda mechi ya kwanza mabao 3-1 itafanikiwa kuitoa Sudan itacheza na Nigeria ambayo yenyewe imefuzu moja kwa moja kucheza raundi ya pili ya michuano hiyo.
 Mechi ya kwanza itachezwa Julai 28 jijini Dar es Salaam wakati ya marudiano itafanyika Nigeria kati ya Agosti 10, 11 na 12 mwaka huu. Fainali za U20 kwa Afrika zitafanyika Machi mwakani nchini Algeria

Post a Comment

Previous Post Next Post