WAKATI timu ya Taifa ya soka ya Wanawake ‘Twiga Stars’
inaondoka kesho kwenda Ethiopia Kampuni ya Bia Serengeti (SBL) kwa kushirikiana na Benki ya NBM, wameichangia
timu hiyo kiasi cha sh.Twiga Stars’ Sh. Milioni 30 ili kuiwezesha timu hiyo.
Twiga Stars itaondoka kwa ndege ya Ethiopian
Airlines kwenda Addis Ababa kwa ajili ya
mechi ya mchujo ya Fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) dhidi ya
Ethiopia, itakayopigwa Mei 27 mwaka huu.
Akizungumza leo katika makabidhiano hayo, yaliyofanyika kwenye
hosteli za Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), Mkurugenzi wa Masoko wa SBL,
Ephraim Mafuru alisema kwamba wameamua kutoa mchango huo baada ya kuombwa na
serikali kuisaidia kutokana na kutokuwa na mdhamini.
Alisema wao wametoa Sh. Milioni 15 na NMB nayo imetoa
kiwango kama hicho, sambamba na vifaa vya michezo vikiwemo jezi, viatu, soksi,
suti na vinginezo vyote vikiwa na thamani ya shilingi mil.5.5.
“Kwa kuzingatia umuhimu wa kuisaidia timu hiyo, tulikutana
na NMB, ambao walikuwa wadhamini wenzetu katika timu ya soka ya wanaume, Taifa
Stars kabla ya kujitoa mwaka jana na tukakubaliana kuisaidia Twiga kwa kiwango
hicho”, alisema.
Naye Meneja Masoko wa NMB, Imani Kajula alisema kwamba kama
wadau wakubwa wa michezo wameona umuhimu wa kuisaidia timu hiyo na pia
kuanzisha kampeni ya kuitafutia misaada zaidi.
Alisema wamefungua akaunti inayoitwa; Changia Twiga Stars na
amewataka wadau na makampuni mengine kuichangia timu hiyo kupitia akaunti hiyo
ambapo anaamini kutokana na benki yao
kuwa na matawi mengi nchini, itakuwa rahisi kwa wadau mbalimbali
kuisaidia timu hiyo.
Kwa upande wake, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Nasra Juma
Mohamed pamoja na kuwashukuru SBL na NMB kwa msaada huo, aliahidi matokeo
mazuri katika mechi yao hiyo.
HAta hivyo,Nasra alisema Watanzania wasikatishwe tamaa na
matokeo mabaya ya mechi zao mbili za majaribio kwani zimewapa ari kubwa na
kuwasaidia kwa kiasi kikubwa kuona ni sehemu gani wanahitaji kuifanyia
marekebisho kabla ya kuivaa Ethiopia.
Nasra pia aliwashukuru Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo
na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dioniz Malinzi walioitembelea
timu hiyo kambini juzi na kutoa posho ya
siku 16 kwa wachezaji na makocha wa timu hiyo.
Awali, Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Sunday Kayuni alisema timu hiyo inakabiliwa na hali mbaya
kifedha hivyo TFF ikaamua kusaka
wafadhili kwa kushirikiana na serikali na akawashukuru SBL na NMB kwa
kujitokeza, huku akiyaomba makampuni mengine kujitokeza kuisaidia timu hiyo ili
iweze kufuzu kwa mara ya pili mfulululizo kucheza fainali hizo.
Msafara wa Twiga Stars utakaokuwa na watu 25 wakiwemo
wachezaji, benchi la ufundi na viongozi utaagwa kesho saa saa tano asubuhi kabla
ya kuondoka saa 11 jioni chini ya Mwenyekiti wa Chama cha soka cha Wanawake Tanzania (TWFA) ambaye pia ni Mjumbe
wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Lina Kessy.
Twiga Stars itarejea nyumbani Mei 28 mwaka huu kusubiri
mechi ya marudiano itakayochezwa Juni 16 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam. Mshindi ndiye atakayepata tiketi ya kucheza Fainali za Nane za AWC
zitakazochezwa Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea.