SHIRIKISHO la soka Tanzania (TFF)
limesogeza mbele kipindi cha kuwasilisha usajili kwa klabu za ligi kuu na ligi
Daraja la kwanza msimu wa 2012/2012 hadi Agosti 15 mwaka huu.Awali zoezi hilo lilikuwa likamilike leo.
Katibu Mkuu wa TFF , Angetile Osiah alisema kwamba marekebisho hayo
yanatokana na mkanganyiko uliojitokeza na kusababisha baadhi ya vilabu
kuchelewa kuwasilisha majina.
Alisema kutokana na mabadiliko
hayo, muda wa siku saba za kuwasilisha pingamizi utakuwa kuanzia Agosti 15 hadi
Agosti 22, 2012, kabla ya kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji
kukutana kupitisha usajili Agosti 24 hadi Agosti 25, 2012.
Alisema klabu zinatakiwa
ziwasilishe usajili pamoja na mikataba ya wachezaji kama
kanuni zinavyotaka na usajili wa kwanza utahusu timu za vijana walio na umri
chini ya miaka 20.
Katibu hiyo pia amezitaka
klabu zote zinazoshiriki ligi kuu na ligi daraja la kwanza kuwasilisha majina
ya viwanja zitakazovitumia kwa ajili ya msimu ujao.
“Pia klabu husika ziwasiliane
na vyama vyao vya mikoa ili viwasilishe maombi ya kutumia viwanja hivyo kwa
mechi za ligi kuu na ligi daraja la kwanza msimu mpya wakati zikisubiri ratiba
kutangazwa”, alionmgeza Osiah