Baraza
la Wazee la klabu ya Yanga, limepongeza uamuzi wa Nchunga kujiuzulu na kuwa,
baada ya zoezi hilo wanasubiri mwongozo toka TFF ili waweze kuendelea na
mchakato mwingine, ukiwemo wa kukabidhi timu kwa baraza la wadhamini ambalo
litasimamia usajili wa wachezaji na mambo mengine.
Hata
hivyo, baraza hilo kupitia kwa Katibu wake, Ibrahim Akilimali, walisema kwamba,
kujiuzulu kwa Nchunga kunamaanisha kuwa, hata wajumbe wengine waliogoma kuachia
ngazi kama walivyowataka, nao hawawatambui kama ni viongozi wa Yanga.
Aliongeza
kuwa, pamoja na kuziuzulu huko, bado wanaendelea na mpango wao wa kufika Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, (TAKUKURU), pamoja na wizara yenye dhamana na
michezo, ili kukagua mali za Yanga, kwani wanaamini kulikuwa na ubadhirifu mkubwa.
Juzi,
Nchunga alitangaza kujiuzulu wadhifa wake huo kufuatia msigano baina yake na
baadhi ya wanachama wa Yanga wakiongozwa na Baraza la Wazee, kumtaka ajiweke
kando kutokana na kushindwa kuiletea mafanikio klabu hiyo, ambayo ilijikuta
ikipokwa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania
Bara uliokwenda kwa mahasimu wao Simba.