WAKATI wajumbe wa kamati ya utendaji ya klabu ya Yanga
wakizuia kujiuzulu kwa mwenzao Mohammed Bhinda (pichan), badala yake wajumbe hao
walimtaka mwenyekiti wa klabu hiyo Lloyd Nchunga kujiuzulu.
Maamuzi hayo yalifikiwa juzi katika kikao cha kamati ya
utendaji ya Yanga kilichoketi kwa ajili ya kujadili mustakabali mzima wa hali
tete inayoendelea ndani ya klabu hiyo, pamoja na barua ya masharti waliyopewa
na aliyekuwa mfadhili wa klabu hiyo Yusuf Manji.
Habari zilizopatikana toka ndani ya kikao hicho zinaeleza
kwamba, baada ya Bhinda kuwasilisha barua yake ya kujiuzulu, wajumbe hao
wakiongozwa na Salum Rupia walizuia zoezi hilo kwa madai ya kwamba kiongozi
huyo ni muhimili mkubwa ndani ya uongozi huo.
Imeelezwa kuwa, pamoja na kugoma huko, wajumbe hao walidai
kuwa ni heri Nchunga ajiuzulu kwani ndiye anayelalamikiwa zaidi na wanachama wa
klabu hiyo lakini si Nchunga hivyo kumshauri aachie ngazi.
Mmoja ya wajumbe hao alieleza kwamba baada ya kumsauri
Nchunga kuachia ngazi aliwaomba wampe
siku mbili au tatu afikirie zaidi ushauri huo kabla ya kutolea uamuzi.
“NI kweli tulizuia barua ya kujiuzulu kwa Bhinda kwani bila
yeye hakuna lolote katika uongozi wa Yanga na tulimshauri Nchunga ajiuzulu
kwani matatizo yote hayo na kelele kutoka kwa wanachama vinamlenga
yeye,”alisema mjumbe mmoja.
“Kama tusipomshauri afanye hivyo itakuwa ngumu kufanuikisha
mambo mengi ambayo yanaikabili timu yetu yanayohitajika kufanyika haraka
iwezekanavyo na kwa hali yake ya kuendelea kuwepo ndani ya Yanga kutafanya
mambo yaendee kuwa magumu zaidi,”aliongeza .
Kikao hicho kilihudhuriwa na wajumbe wachache baada ya wengi
wao kutangaza kubwaga manyanga kutokana na kuchoshwa na hali ya sintofahamu
inayoendelea ndani ya klabu hiyo, ambapo tayari
Makamu Mwenyekiti Davis Mosha, pamoja na wajumbe Seif Ahmed, Ali Mayay,
Bhinda na Mzee Yusuf walitangaza kung’atuka
Kwa sasa Yanga imebaki na wajumbe wanne, wakimo Sarah Ramadhani,Tito Osoro, Charles Mgondo,
na Salum Rupia.
Hata hivyo, Nchunga ambaye jumapili iliyopita alivuliwa
madaraka hayo na wanachama zaidi ya 700 waliokutana makao makuu ya klabu hiyo
iliyopo mitaa ya Jangwani na Twiga, hakupatikana kuzungumzia suala hilo baada
ya simu yake kuita bila kupokelewa.
Hivi karibuni, uongozi wa Yanga ulijikuta katika msigano na
wanachama wa Yanga wakiongozwa na baraza la wazeee na baadhi ya vijana wakitaka
ujitoea madarakani kutokana na kushindwa kuiletea mafanikio timu hiyo ambayo
ilijikuta ikiutema ubingwa wake wa ligi kuu bara ulionyakuliwa na mahasimu wao
Simba na yenyewe kuishia nafasi ya tatu.
Aidha, uongozi huo unadaiwa kushindwa kuwalipa wachezaji
pamoja na viongozi wa benchi la ufundi hatua ambayo imepelekea benchi la ufundi
kuachia ngazi, huku klabu hiyo ikiwa mbioni kutaifishwa na mahakama kuu baadhi
ya mali zake kutokana na deni la milioni 106.
Tayari Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilikemea mapinduzi
yaliyofanywa na wanachama wa Yanga kwa madai ya kukiuka kanuni, huku wakidai
kutotambua mapinduzi hayo na kuwataka wanachama hao kutumia busaya katika
kutatua suala hilo.
Hata hivyo, wazee hao wametishia kuifuta Yanga TFF na
kuihamishia Visiwania Zanzibar, pia kuwasilisha ombi maalum kwa taasisi ya
kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) ili imchunguze Nchunga kwa madai kuwa
huenda kuna ubadhirifu anaoufanya ndiyo maana hataki kung’oka Yanga.
Mpendwa tupo pamoja, ni hapa na pale twashukuru kwa taarifa hii
ReplyDelete