MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, leo imeshindwa kuanza kusikiliza kesi ya wizi wa madini ya shaba yenye
thamani ya sh milioni 400, inayomkabili Katibu wa zamani wa Simba, Hassan Othman 'Hassanoo' (43) na wenzake watatu.
Hiyo imetokana na wakili wa serikali aliyekuwa akiindesha
kesi hiyo tangu awali, Elizabeth Kaganda kuwakabidhi jukumu hilo mawakili wengine kwani yeye ametingwa na
majukumu mengine.
Mbele ya Hakimu Mkazi Devotha Kisoka, mawakili wapya
wanaoendesha kesi hiyo, Theophil Mtakyawa na Ester Kyala, waliieleza mahakama
kuwa, kesi hiyo jana ilikuja kwa ajili ya mashahidi wa upande wa jamhuri kuanza
kutoa ushahidi.
Hata hivyo, walisema hilo
halitawezekana kwa sababu wakili wa serikali (Kaganda), aliyekuwa akiendesha
kesi hiyo amewakabidhi wao kuiendesha kwa kipindi chote kutokana yeye kupewa
majukumu mengine ya kiserikali.
“Na leo asubuhi ndiyo tumekabidhiwa jalada la kesi
hii, hivyo hatujajiandaa kabisa, tunaomba mahakama itupatie muda ili twende
tukalisome jalada hii tufahamu vizuri kesi hii,” alidai wakili Mtakyawa.
Hakimu Kisoka alikubaliana na ombi hilo na akaahirisha kesi hiyo hadi Julai 25,
maka huu itakapokuja kutajwa na Agosti 6-7 itaanza kusikiliziwa.
Katika hati ya mashitaka, wanadaiwa Agosti 28 mwaka 2011
jijini Dar es Salaam, washitakiwa hao kwa pamoja, walipanga njama ya kuiba mali
hizo.
Shitaka la pili, tarehe hiyo hiyo, washitakiwa hao waliiba
tani 26 za madini ya shaba
yenye thamani ya fedha hizo yaliyokuwa yanasafirishwa kutoka Zambia kuja
nchini.
Ilidaiwa kuwa, madini hayo yalikuwa yanasafirishwa kwenye
lori lenye namba za usajili T 821 BCL na tela namba T 566 BCL ambayo ni mali ya Kampuni
ya Liberty Express.
Katika shitaka la tatu, wanadaiwa washitakiwa hao walipokea mali hiyo huku
wakijua kuwa ni ya wizi.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Wabura Magenga (32),
Dk. Najim Msenga na Salim Shekibala.