NAHODHA wa timu ya Taifa ya Wanawake ‘Twiga
Stars’ Sophia Mwasikili anatarajiwa kuwasili nchini keshokutwa tayari kwa mchezo
baina ya timu hiyo na Ethiopia utakaopigwa juni 16 mwaka huu.
Mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya pili
ya michuano ya Afrika kwa Wanawake (AWC) ni mahususi kwa ajili ya kuwania
tiketi ya kucheza fainali zitakazofanyika Novemba mwaka huu nchini Equatorial
Guinea.
Ofisa habari wa Shirikisho la soka Tanzania
(TFF) Boniface Wambura amesema leo kwamba awali nyota huyo anayecheza soka la
kulipwa katika klabu ya Luleburgargusu ya Uturuki awali ilikuwa atue nchini
jana lakini ilishindikana baada ya kuchelewa ndege.
Alisema benchi la ufundi bado linamuhitaji
mchezaji huyo kutokana na mchango wake katika kikosi hicho kilichopo kambini
katika hosteli ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Kibaha, Pwani kikiendelea na
maandalizi yake ya mchezo huo.