Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Leodegar
Tenga amekataa barua ya kuomba kujiuzulu ya mjumbe wa Kamati ya Sheria, Maadili
na Hadhi za Wachezaji ya TFF, Ismail Aden Rage.
Rage ambaye pia ni Mwenyekiti wa klabu ya Simba alimuandikia
Rais Tenga barua ya kujiuzulu wadhifa huo kwa kile alichosema ‘kamati hiyo
kushindwa kwa makusudi kusimamia sheria na kanuni za uendeshaji wa mpira Tanzania
zinavyoeleza.’
Amekataa ombi hilo kwa maelezo kuwa kama Rage amehisi kuwepo
udhaifu wa kutosimamia sheria na kanuni kama inavyotakiwa, ni vyema akaendelea
kuwemo kwenye kamati hiyo ili kuisaidia kusimamia sheria na kanuni hizo kama
inavyotakiwa badala ya kujiuzulu.
“Kutokana na uzoefu na uwezo ambao Rage anao katika uongozi
wa mpira wa miguu, ni vyema akautumia kuisaidia kamati kutekeleza wajibu wake
kama inavyotakiwa kwa mujibu wa sheria ili kusaidia kusukuma mbele gurudumu za
maendeleo ya mpira wa miguu,” amesema Rais Tenga.
Pia Rais Tenga amesisitiza kuwa ni muhimu kwa mpira wa miguu
kuongozwa kwa kufuata sheria na kanuni zilizopo, rai ambayo imetoa kwa kamati
zote za TFF ili kuhakikisha kuwa mpira wa miguu unaongozwa bila kuonea wala
kupendelea upande wowote.
Rais Tenga amesisitiza kuwa kamati hazina budi kuchukua
hatua zinazostahili bila woga pale kanuni zinapotaka hatua kuchukuliwa.
Amezitaka kamati zisisite kwa namna yoyote ile kuchukua hatua kwa vile kwa
kufanya hivyo, uwezekano wa kutokea upendeleo au uonevu utapungua, hivyo mpira
wa miguu kuongozwa kwa sheria na haki.